Meta kuachia programu mpya ya ‘Thread’ hivi karibuni

June 19, 2023 12:52 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Inatarajiwa  kuchochea mazungumzo na kuimarisha uhusiano.
  • Itakuwa mshindani wa jukwaa la Twitter kwani vitu vingi vinafanana.

Dar es salaam. Kampuni ya teknolojia ya Meta inayomiliki mitandao ya Facebook, Instagram pamoja na WhatsApp, inajiandaa kuzindua program mpya ya Thread inayotarajiwa kuchuana na jukwaa maarufu la Twitter.

Program hiyo itawawewezesha watumiaji wa mtandao wa Instagram kutuma na kusoma ujumbe mrefu kama ilivyo katika mtandao wa Twitter unaomilikiwa na mfanyabiashara bilionea Elon Musk.

Mark Zuckerberg ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Meta  alipokuwa akizungumza na umati wa watu hivi karibuni na aliwaambia kuwa program hiyo itachochea mazungumzo yenye nguvu na kuimarisha uhusiano.

“Leo, tunawasilisha Thread, program mpya inayowakutanisha watu kupitia mazungumzo yenye maana…tunaamini ni wakati wa kuunda jukwaa ambalo halisaidii tu watu kushiriki mawazo yao kwa ujumbe mfupi, bali pia linalochochea mazungumzo yenye nguvu na kuimarisha uhusiano.” amesema Zuckerberg

Kuzinduliwa kwa program hii ni mwendelezo wa ushindani kati ya kampuni ya za teknolojia na mawasiliano zilizopo duniani katika kuhakikisha watumiaji wanafurahia na kurahisishiwa mawasiliano yanayofanyika kwa njia ya mtandao.

Hivi  karibuni Meta walibadilisha muonekano wa jukwaa la Instagram ili kufanana kwa ukaribu na jukwaa pinzani la TikTok linalokua kwa kasi, pia walizindua kipengele kipya cha ‘Channel’ kwenye jukwaa la WhatsApp kinachofanana na Telegram kama njia kwa watu binafsi au mashirika kusambaza jumbe kwa watu wengi zaidi.

Utofauti wa Thread na Twitter.

Program mpya ya Thread itakayozinduliwa hivi karibuni inakuja na mambo mapya ikiwemo matumizi ya uhalisia pepe, na faragha iliyo imarishwa. 

‘Tread chains’

Moja ya huduma za kuvutia zaidi katika program mpya ya Meta ni ‘Thread Chains,’ ambayo inawaruhusu watumiaji kuunganisha mazungumzo yanayohusiana.

Pia wataweza kuunda mwendelezo mzuri wa mawazo na fikra hivyo itafanya iwe rahisi kwa watumiaji kupitia na kuchunguza maoni mbalimbali kuhusu mada fulani,  tofauti na mazungumzo ya moja kwa moja yaliyozoeleka katika mtandao wa Twitter.


Soma zaidi


Zaidi ya hayo, Thread inaleta mfumo mpya wa kushiriki, ukibadilisha ‘likes’ za Twitter na kukaribisha njia tofauti za kuelezea hisia. Watumiaji watapata fursa ya kuonyesha shukrani, kutokubaliana, kuelewa, na kusaidia. Huduma hii inalenga kuchochea mawasiliano yenye maana, kukuza uelewa na mshikamano wa jamii ya kupitia mtandao.

Uhalisia pepe (Virtual realities)

Aidha, Thread inajumuisha teknolojia ya Visual Reality (VR) ya Meta, ikiruhusu watumiaji kufaidi uzoefu wa sauti, picha na video kwa digrii 360, yaani unaweza kushiriki matukio ya moja kwa moja pamoja na mijadala ya kuvutia iliyoundwa na watumiaji wengine. 

Hii itasaidia kufungua njia mpya za uzoefu wa pamoja, zikivuka mipaka ya mawasiliano ya kawaida ya maandishi.

Faragha iliyoimarishwa

Wakati programu hiyo ikiwa tayari kwa uzinduzi, Meta pia imeweka kipaumbele cha faragha ya watumiaji na kupambana na habari potofu. 

Program hiyo italeta zana imara za kudhibiti maudhui, kwa tumia uwezo wa akili bandia zitakazoweza kutambua na kuondoa taarifa zisizo sahihi au hatari kwa haraka.

Je, Thread itakuwa jukwaa jipya la mazungumzo ya mtandaoni na majadiliano yenye kuvutia zaidi? Ni wakati tu utakaoonesha ikiwa bidhaa mpya ya Meta inaweza kuzidi umaarufu wa Twitter na kubadilisha mustakabali wa mitandao ya kijamii.

Chris Cox ambaye ni Afisa Mkuu wa bidhaa katika kampuni ya Meta,  amesema lengo la program hiyo ni kuwaongezea usalama watumiaji wa na urahisi wa kutumia.

“Lengo la kampuni kwa programu hii ni “usalama, urahisi wa kutumia, kutegemewa” na kuhakikisha kuwa watumiaji  wana mahali pazuri pa kujenga na kukuza hadhira yao.” amenukuliwa Cox katika tovuti ya The Verge.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW