Kozi za kipaumbele maombi ya mikopo elimu ya juu mwaka 2023-24
- Ni pamoja na programu za ualimu wa masomo ya sayansi na sayansi za afya.
- Serikali yatenga Sh731 bilioni kwa ajili ya wanufaika.
Dar es Salaam. Mkopo wa elimu ya juu ni ndoto ya wanafunzi wengi wanaotarajia kusoma kuanzia ngazi ya elimu ya shahada, katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Tanzania.
Serikali iliweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaotoka familia zenye kipato cha chini ili kumudu gharama za masomo, ingawa kutokana na uhaba wa fedha si wanafunzi wote watokao katika familia duni hufanikiwa kupata mkopo.
Kiwango cha mkopo hutofautiana kulingana na kozi ambayo mwanafunzi anasoma, mathalani wanafunzi wanaosoma kozi za udaktari hutajwa kuwa ndio wanaopokea kiwango kikubwa cha mikopo.
Ikiwa wewe ni mhitimu wa kidato cha sita au diploma unayetarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu mwaka huu, ni muhimu kufahamu kozi zitakazopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo jambo litakalokusaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuomba mikopo pamoja na vyuo.
Kozi hizo zitakazopewa kipaumbele zimeainishwa katika muongozo wa utoaji mkopo na ruzuku kwa wanafunzi uliozinduliwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga Julai 13, 2023.
Akizungumzia muongozo huo Naibu Waziri amesema Serikali imetenga Sh731 bilioni zitakazowanufaisha wanafunzi 205,000 katika mwaka wa masomo 2023-2024. .
Kwa mujibu wa mwongozo huo, kozi hizo zitakazopewa kipaumbele kwa mwaka huu zimegawanywa katika makundi matatu ili kuakisi vipaumbele vya Taifa.
Soma zaidi
Masomo ya sayansi kipaumbele cha kwanza
Kundi la kwanza la wanafunzi watakaopewa kipaumbele ni wale watakaosoma kozi za ualimu wa sayansi (Fizikia, Kemia na Biolojia), ualimu wa hisabati na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Pia Sayansi za Afya, Uhandisi, Jiolojia ya Petroli, Sayansi ya Kompyuta, Kilimo, Sayansi ya wanyama na Uzalishaji, Takwimu bima, Sanaa katika kiswahili na Elimu ya ufundi.
Kundi la pili la watakaonufaika na mikopo hiyo ni wale ambao kozi zao zitajikita katika Programu za msingi za Sayansi ikiwemo sayansi ya wanyama, mimea, Kemia, na Fizikia pamoja na sayansi za ardhi inayohusisha ubunifu wa majengo.
Kundi la tatu na la mwisho la wanaufaika hao litahusisha kozi zinazohusu sayansi za jamii zinazojumuisha masomo ya Biashara na Uongozi, Uhasibu, Masoko, Fedha, Uchumi, Takwimu, Mazingira, Maendeleo ya Jamii, na Ustawi wa Jamii.
Pia masomo ya Maendeleo, Sosholojia, Sayansi ya Siasa, Sanaa, uchoraji, Sayansi ya Ubunifu, Muziki, Sheria, Lugha, Fasihi, Jiografia, Saikolojia, Anthropolojia, Akiolojia na masomo ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano.
Aidha bodi hiyo imesema dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao (Online Loan Application Window) litakua wazi kwa siku 90 kuanzia Julai 15 hadi Oktoba 15 mwaka huu.
Kwa wanafunzi wanaoendelea na mafunzo katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Naibu Waziri Kipanga amesema tayari Heslb imeshafanya mawasiliano rasmi na makao makuu ya JKT ili kuwapatia elimu ya uombaji sahihi kupitia ‘Mwongozo Rafiki’.