Kutana na kuku anayeuzwa Sh800,000 Tanzania

July 5, 2023 6:40 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuku mmoja anaweza kuwa na uzito wa kilo tisa hadi 12.
  • Ndani ya miezi saba mpaka mwaka mmoja anaweza kufikisha zaidi ya kilo 9.
  • Ni chanzo kizuri cha ajira kwa vijana na wafugaji wa kuku.

Dar es Salaam. Katika moja ya mabanda ya maonyesho ya biashara ya Saba saba jijini Dar es Salaam, kundi kubwa la watu zaidi ya 10 limemzunguka mmoja wa wafanyabiashara anayefuga kuku wajulikanao kama Brahma.  

Watu waliopo hapa wapo bize kuwapiga picha kuku na kumsikiliza Sebastian Massawe muuzaji wa kuku hao wa aina yake ambao hufikia hadi uzito wa kilo 12. 

Huyu ni kuku gani mkubwa hivi? Hawa kuku unawauzaje? Wana tofauti gani na kuku wa kawaida? 

Haya yalikuwa ni sehemu ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa mara kwa mara na watembeleaji wa banda la  Massawe ambaye amekuwa akiwafuga kuku wa aina hiyo kwa miaka 15 sasa.

Kuku anaowauza Massawe wana kimo cha zaidi ya sentimita 76.2 sawa na urefu wa zaidi ya rula mbili zilizounganishwa zenye urefu wa sentimita 30 kila moja. 

Kuku hao wana manyoya mengi yanayofunika hadi miguuni, uzito wa zaidi ya kilo 9 pamoja na mwendo wa madaha ambao umekuwa kivutio kikubwa katika  Maonyesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.

‘Brahma Rosters’, kwa mujibu wa Massawe, ndio jina la kitaalamu waliopewa kuku hao kutoka nchini Ujerumani wanaosifika kwa kutaga mayai mengi na kuwa na nyama nyingi inayoweza kuliwa katika sherehe au mikusanyiko mbalimbali.

Massawe ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa bei ya kuku hao ipo juu zaidi ya kuku wa kienyeji.

“Kuku wa kienyeji akiwa mkubwa sana bei yake inaweza kufika hadi Sh15,000 lakini huyu kuku hawa bei yake inafika hadi Sh1.6 milioni,” anasema Massawe huku akiwaonyesha kuku wawili mkononi mwake wakati akiwaeleza watembeleaji wake. 

Gharama ya kuku mmoja wa Brahma ni wastani wa Sh800,000 sawa na kuku 114 wa kawaida wa kisasa wanaouzwa Sh7,000 katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam.

Mayai ya kuku hao huuzwa kwa Sh30,000 kwa yai moja huku vifaranga vya wiki tatu hadi mwezi mmoja vikiuzwa kuanzia Sh100,000 hadi Sh150,000.

Kufuatia bei hiyo, baadhi ya wakazi na wafanyabiashara wa chakula jijini Dar es Salaam wamesema si rahisi kwa watu wa kipato cha chini kumudu gharama. 

“Mimi nimezoea kununua kuku kwa Sh7,000 na ikiwa wa kienyeji hadi Sh15,000…huyo kuku wa Sh800,000 sitaweza kumudu kutokana na aina ya wateja tulionao katia maeneo haya,” anasema Bakari Mussa muuza chakula Mwananyamala jijini Dar es Salaam. 

Kwa mama wa nyumbani kama Rose Mathias beihiyo ya kuku anasema siyo rafiki kwa kuwa watu wengi wana kipato cha chini. 

“Unakuta mahitaji ya nyumbani unatumia Sh20,000 halafu unakuja tena kusikia kuna kuku wa Sh800,000… hiyo bei ipo juu sana,” anasema Rose.

Kuku aina ya Brahma wakiwa kwenye mabanda yao yaliyopo Maonyesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.Picha|Daudi Mbapani/Nukta Africa.

‘Utunzaji wa Brahma ni rahisi tu’

Mfugaji huyo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika ufugaji wa aina mbalimbali za kuku anasema utunzaji wa kuku hao ni rahisi na  hautofautiani sana na ule wa kuku wa kienyeji.

Anasema kuku mmoja anaweza kula robo tatu ya kilo au gramu 750 kwa siku na unaweza kumuachia ajitafutie chakula wenyewe kinachotosheleza mahitaji yake ya siku.

“Utunzaji wake ni kama kuku wa kawaida kama unashamba lako unamuachia anajitafutia chakula mwenyewe … anapata chanjo kama kuku wa kawaida,” ameongeza.

Hata wakati mfugaji huyo akieleza urahisi wa ufugaji huo tovuti ya Chickens and more inasema ufugaji wa ina hii ya kuku unaweza kuwa gharama zaidi kutokana na kuku hao kula sana kuliko wa kawaida.

“Wakipata njaa kuku hawa huwa na tabia ya usumbufu kwa kuku wengine hivyo ni bora kuhakikisha muda wote hawana njaa,” imesema tovuti hiyo.

Mbali na hayo tovuti hiyo imewataja kuku hao kama moja ya ina ya kuku watulivu wasio na kelele nyingi wala usumbufu kwa mfugaji.


Zinazohusiana


Ni chanzo cha ajira

Kwa vijana wanaotafuta ajira, ufugaji na uuzaji wa kuku hawa unaweza kuwa fursa mpya ya ajira kutokana na aina yake kutokuwepo maeneo mengi na gharama yake kuwa juu.

Kuku hao ambao kwa sasa wanapatikana hapa nchini wanaweza kukuingizia faida inayoweza kukusaidia kumudu gharama za maisha kwa kuwa Massawe anasema soko lake lipo la kutosha.

“Kwa siku, napokea oda ya vifaranga 30 hadi 50, kwa hiyo kila mwezi nauza hadi kuku 200….kila mwezi nafunga hesabu ya Sh4 milioni au zaidi,” anasema.

Ikiwa unatamani kuanza kujiajiri kupitia ufugaji huo, Massawe anayepatikana Mkuranga mkoani Pwani anasema unaweza kuunua vifaranga vya kuku hao kwa kuanzia Sh100,000 kisha ukapata elimu ya ufugaji inayotolewa na kituo chao.

Enable Notifications OK No thanks