Mambo yatakayozisadia nchi za Afrika kuongeza mapato ya kodi
- Ni pamoja na kuitambua sekta isiyo rasmi na kodi za madini na gesi.
- Mikakati kujadiliwa katika mkutano wa Jukwaa la Kodi Afrika (ATAF) 2023.
Dar es Salaam. Mataifa ya Afrika yanatarajia kuja na mikakati mipya ya ukusanyaji wa kodi ikiwemo kukusanya kodi katika sekta isiyo rasmi ili kuongeza mapato yatakayosaidia kutokomeza umaskini katika nchi hizo.
Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo amewaambia wanahabari leo kuwa mikakati hiyo ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano wa Jukwaa la Kodi barani Afrika (ATAF) unaofanyika nchini.
“Baadhi ya maeneo ambayo tutajadili ni pamoja na kukusanya mapato kutoka kwenye sekta isiyo rasmi, katika sekta ya madini na gesi, kujenga mifumo ya kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kujenga uhiyari wa kulipa kodi,” amesema Kayombo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kayombo, ukubwa wa sekta isiyo rasmi katika nchi za Afrika unachangia upotevu wa mapato kwa kiasi kikubwa kwa kuwa idadi kubwa ya wanaojihusisha nayo hawajajisajili na ni vigumu kuwafuatilia na kukusanya kodi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa nane wa ATAF jijini Dar es Salaam. Picha l TRA
Muhtasari wa taarifa ya tathmini ya sekta isiyo rasmi nchini Tanzania wa mwaka 2018 unabainisha kuwa sekta isiyo rasmi katika shughuli za kiuchumi nchini Tanzania ni asilimia 92.8 ambapo mjini ni asilimia 30.8 na vijijini ni asilimia 60.
Aidha, bajeti ya Tanzania mwaka 2023/24 inaonesha Sh26.73 trilioni sawa na asilimia 60 ya fedha inayokusudiwa kutumika itatoka kwenye mapato ya kodi.
Soma zaidi
Hii inamaanisha kuwa kama Serikali itaitambua sekta isiyo rasmi na kuanza kukusanya kodi, mchango wa sekta hiyo kwenye bajeti ya Taifa utaongezeka jambo litakalopunguza kutegemea mikopo na misaada ya wafadhili kwenye bajeti kuu.
Kayombo ameongeza kuwa matokeo ya utafiti yanaonesha matatizo ya kodi yanafanana katika nchi nyingi za Afrika hivyo mkutano huo utakuwa na tija kwa kuwa utatoa suluhu za matatizo hayo.
Kwa upande wake Carolina Mutayabarwa, msimamizi wa mafunzo kutoka Jukwaa la Kodi barani Afrika (ATAF) amebainisha kuwa miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano wa mwaka huu ni pamoja na namna mataifa ya Afrika yanavyoweza kukusanya kodi kutoka kwenye mazingira.
“Kuna nchi ambazo zimeanzisha kodi ya uchafuzi wa mazingira (carbon taxation) wanatoza kodi kutokana na namna mazingira yanavyoharibiwa kwa kutoa gesi ya kaboni, hilo ni eneo jipya ambalo halijawa na tafiti nyingi hivyo tutakwenda kuziangazia katika mkutano huu,” amesema Mutayabarwa.
Mkutano huo wa siku tatu ambao unafanyika kwa mara ya nane, umendaliwa na ATAF kwa kushirikiana na TRA ambapo wakuu wa taasisi za kodi, watafiti, wawakilishi wa taasisi za elimu na wadau wa kodi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika hukutana kujadili mustakabali wa sekta hiyo muhimu.
Latest