Tanzania itakavyonufaika na Katiba Tume ya Usafiri wa Anga Afrika

August 31, 2023 7:40 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuimarika kukua kwa uchumi na kuimarika kwa usalama wa nchi
  • Serikali yatakiwa kusimamia matakwa ya katiba ili kupata matokeo chanya

Dar es Salaam. Agosti 30, 2023, Bunge la Tanzania, liliidhinisha azimio la katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC), hatua inayotarajiwa kuongeza manufaa kupitia sekta ya anga ikiwa ni pamoja kukua kwa uchumi.

Mwaka 2009 AFCAC ilifanyia marekebisho katiba yake ya mwaka 1969 na kuanza kutumika Mei 11, 2010 ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ziliipitisha katiba hiyo mwaka 2019 na kuanza kuitumia mwaka 2020.

Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi alipokuwa akisoma hotuba ya kuridhia azimio hilo amewaambia wabunge kuwa kwa sasa Tanzania si mwanachama wa umoja huo kwani bado haijaridhia katiba mpya iliyotambuliwa.

“Kwa kuzingatia manufaa yatakayopatikana kwa kuridhia katiba mpya ya tume ya usafiri wa anga ya Afrika ya mwaka 2009, Bunge katika mkutano wake wa 12 linaadhimia kuridhia katiba mpya” amesema Profesa Mbarawa jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Mbarawa, baadhi ya manufaa yanayotarajiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama wa nchi, kuongezeka  kwa ufanisi kupitia mafunzo yanayo ratibiwa  kimataifa, pamoja na  kuongezeka kwa  idadi ya wataalamu na tafiti zinazohusiana na masuala ya anga. 

Ikumbukwe kuwa Tanzania imeridhia katiba mpya wakati jitihada za kuliongezea nguvu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili lizalishe faida zikiendelea kuchukuliwa.

Juni 3, 2023 ATCL ilipokea ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54 za mzigo na kulifanya shirika hilo kuwa na jumla ya ndege 13 zikiwemo ndege mbili za Boeing 787 Dreamliners.

Kuridhiwa kwa azimio la katiba mpya kunaweza kuchangia ukuaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kuwezesha kubadilishana mbinu bora na uzoefu wa kimataifa, mipango ya kujenga uwezo, na kutetea maslahi ya nchi katika ngazi ya kikanda na kimataifa.


Soma zaidi


Abubakar Asenga, Mbunge wa Kilombero alipokuwa akichangia hoja kuhusiana na azimio hilo amebainisha  kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi kwa kutengeneza ajira na kukuza sekta ya usafiri wa anga, kwa kuwa mashirika ya ndege yataweza kufanya kazi nchini.

Aidha, Mpango Mkakati wa Wakala wa Uangalizi wa Usalama na Ulinzi wa Anga wa Afrika Mashariki (EAC CASSOA) unabainisha kuwa faida nyingine ni pamoja na kukuza utalii na kupanua wigo wa ushiriki wa nchi katika masuala yanayohusu usafiri wa anga kwenye jukwaa la kimataifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya miundombinu Selemani Kakoso, katiba hiyo  mpya imetungwa ili kutatua changamoto za utekelezaji na mapungufu yaliyobainika katika katiba ya awali.

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu ameitaka serikali kuhakikisha usimamizi wa utekelezaji wa masuala yanayohusiana na katiba iliyoridhiwa, ili kuhakikisha fursa za ukuaji wa ATCL na sekta ya anga kiujumla.

AFCAC ni wakala wa Umoja wa Afrika wenye makao yake makuu jijini Dakar, Senegal, ikiwa na madhumuni ya kuendeleza na kusimamia usafiri wa anga barani Afrika.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV