Saba wakamatwa kwa udanganyifu mitihani darasa la saba Mwanza
- Watuhumiwa hao ni walimu wanne na wanafunzi watatu
- Wote wamekamatwa na watapelekwa mahakamani hivi karibuni
Mwanza. Wiki moja mara baada ya kumalizika kwa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi nchini, Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu saba wakiwemo wasimamizi wa mitihani wanne na wanafunzi watatu kwa tuhuma za udanganyifu.
Watu hao wanatuhumiwa kwa kosa la kuruhusu wanafunzi watatu wa sekondari kufanya mitihani kwa niaba ya wanafunzi wa shule ya msingi waliotakiwa kufanya mitihani hiyo, jambo ambalo ni kinyume na sheria za mitihani.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amewaambia wanahabari leo Septemba 21, 2023 watu hao wanadaiwa kufanya udanganyifu katika Shule ya Msingi Igulumuki iliyopo katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
“Baada ya kamati hiyo kutembelea shule kwa ajili ya ukaguzi ndipo wakabaini kufanyika kwa udanganyifu huo, watuhumiwa walikamatwa na wamehojiwa kwa kina, watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya upelelezi kukamilika,” amesema Mutafungwa.
Soma zaidi
-
Tanzania yasaka Sh8 trilioni kukamilisha mradi SGR
-
Maboresho mapya ya WhatsApp Business kurahisisha biashara za mtandaoni
Wanaotuhumiwa kwa kosa hilo ni wasimamizi wanne wa mitihani hiyo akiwemo mwalimu wa Shule ya Sekondari Sima, Maiko Sheusi (35), Nisa Mwashihava, 38, (mwalimu wa Shule ya Sekondari Kilabela), Bonas Balozi, 33, (mwalimu wa Shule ya Sekondari Buzila Soga) na Azizi Mohamed (36) mwalimu taaluma wa Shule ya Msingi Igulumuki.
Wanafunzi walioshiriki katika udanganyifu huo ni pamoja na Shadrack Bwana (14), Revocatus Paulo(14), na Pendo Bukoma(14), wote wakiwa ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sima.
Udanganyifu katika mitihani ya kitaifa ni miongoni mwa masuala yanayoliumiza kichwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutokana na kujirudia mara kwa mara licha ya adhabu kali zinazotolewa.
Itakumbukwa kuwa Septemba 12 mwaka huu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Ally Mohamed alitoa onyo kwa watakaobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba.
Alisema Baraza lake halitasita kufuta matokeo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wote watakaoshiriki katika udanganyifu.
“Tunaamini wanafunzi wameandaliwa vyema katika kipindi chote cha miaka saba, hatutegemei kuona watahiniwa wanafanya udanganyifu kwa kuwa tutawafutia matokeo,” amesema Dk. Ally.