Fahamu sababu za Rais Samia kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu

December 28, 2023 10:24 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na mageuzi ya kiuchumi pamoja na umahiri katika diplomasia.
  • Aelekeza shahada yake kwa wafanyakazi wa sekta ya utalii na kwa Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Karume.
  • Afikisha jumla ya shahada tatu za heshima za uzamivu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Utalii na Usimamizi wa Masoko na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) huku mchango wake kwenye utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii ukitajwa kama sababu.

Makamu wa Rais wa Suza Dk. Hashim Hamza Chande aliyekuwa akizungumza katika hafla ya mahafali ya 19 ya chuo hicho amewaambia wahudhuriaji leo Disemba 28, 2023 kuwa Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo kwa kuzingatia kifungu cha saba cha Sheria namba nane ya Mwaka 1999 ya Sheria za Suza inayosimamia utoaji wa shahada hizo.

“Uongozi wa Suza umeona kuna haja ya kumtunuku Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan shahada hii, kutokana na mchango wake katika kuinua uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia sekta ya utalii,” amesema Chande.

Chande amebainisha kuwa Rais Samia alifanya juhudi za makusudi kuchechemua sekta ya utalii iliyokuwa imezorota mara baada ya janga la Uviko-19 kutokana na hatua za kujikinga na ugonjwa huo zilizochukuliwa na mataifa ikiwemo kuzuia safari za kimataifa.

“Dk. Samia Suluhu Hassan bila kujali cheo chake akiwa Rais alishiriki mwenyewe kutengeneza filamu ya ‘The Royal Tour’…ikiwa ni programu maalumu ya kimkakati iliyolenga kuionesha dunia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji,” amebainisha Chande.


Soma zaidi : DCEA yakamata kilo 3,182 za dawa za kulevya Tanzania


Kwa mujibu wa Chande, filamu hiyo ilisaidia kuongeza idadi ya watalii nchini Tanzania ambapo waliongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 mpaka kufika watalii milioni 1.4 sawa na ongezeko la asilimia 57.7.

Aidha, takwimu za Wizara ya Utalii zinabainisha kuwa, kwa upande wa Zanzibar watalii waliongezeka na kufikia 548,503 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 39.1 ukilinganisha na waliokuwepo mwaka 2021.

Chande ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2023, idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar imefikia 568,312 sawa na ongezeko la asilimia 18 ukilinganisha na watalii waliotembelea kipindi kama hicho mwaka 2022 jambo lililochangia kuongezeka kwa mapato ya utalii visiwani humo kwa asilimia 93.

“Kutokana na mchango wa utalii, ukuaji wa uchumi wa Zanzibar umeongezeka, kutoka GDP 1.3 mwaka 2020 hadi wastani wa GDP 5.1 mwaka 2021, kiwango cha ongezeko la ukuaji wa uchumi kimekua kwa wastani wa asilimia GDP 6.8 mwaka 2022,” ameongeza Chande.


Soma zaidi : HESLB yaongeza kozi nne za kipaumbele mikopo ya diploma 2023-2024


Utalii ni miongoni mwa sekta nyeti nchini Tanzania kutokana na umuhimu wake ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2022 sekta hiyo ilichangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 21 ya Pato la Taifa.

Sababu nyingine zilizotajwa na Chande hadi kutoa shahada hiyo ni umahiri wa Rais Samia katika diplomasia, jambo lililofungua fursa za uwekezaji pamoja na uwezo wa kusimamia mipango mikakati ya kimaendeleo ya kitaifa na kusababisha mageuzi ya kiuchumi na kielimu.

Itakumbukwa kuwa shahada hiyo, inamfanya Rais Samia kuwa na shahada tatu za heshima za uzamivu alizozipata ndani ya miaka miwili ambapo ya kwanza alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  Novemba 30, 2022 na ya pili alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India Oktoba 10, 2023.

Kwa upande wake Rais Samia amewaambia Watanzania kuwa anaielekeza shahada hiyo kwa watu wote wanaofanya kazi katika sekta ya utalii, pamoja na Rais mstaafu wa sita wa Zanzibar Amani Abeid Karume ambaye ni mlezi wake katika masuala ya uongozi na siasa.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV