Waliofariki kwa ajali mkoani Arusha wafikia 25

February 25, 2024 11:38 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kati ya idadi ya waliofariki wanaume ni 14, wanawake ni 10 na mtoto mmoja.
  • Majeruhi, mashuhuda waeleza ajali ilivyotokea.

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliofariki katika ajali iliyohusisha magari manne yaliyogongana katika barabara kuu ya Arusha – Namanga iliyopo katika eneo la Kibaoni Ngaramtoni mkoani Arusha imefikia 25 huku majeruhi wakiwa 21.

Kati ya idadi ya waliofariki wanaume ni 14, wanawake ni 10 na mtoto mmoja, kwa upande wa majeruhi waliohusika katika ajali hiyo wanaume ni 14 na wanawake ni saba.

Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo Cp Juma awadhi Haji aliyekuwa akizungumza na wanahabari alipotembelea katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha, Mount Meru, jana usiku 24 Februari, 2024 amesema chanzo cha ajali hiyo ni Lori kupoteza uelekeo.

“Chanzo cha ajali hiyo katika uchunguzi wa awali inaelezwa kwamba gari hilo (lori) lilifeli breki na hatimaye kumshinda dereva na kupoteza uelekeo hatimaye kwenda kugonga magari yaliyo mbele yake,” amesema CP Haji.

Magari mengine yaliyohusishwa kwenye ajali iliyotokea saa 11 jioni, Februari 24 mwaka huu ni pamoja na Gari la Shule (school bus) mali ya Shule ya New Vision aina ya Toyota costa, dalala inayofanya safari zake kati ya Arusha mjini na Ngaramtoni, gari ndogo aina ya Mercedes Benz Saloon pamoja na Lori mali ya Kampuni ya KAY ya nchini Kenya.


Soma zaidi:Ajali za barabarani zaongezeka kiduchu, vifo vyafikia asilimia 63


Majeruhi, mashuhuda waeleza ajali ilivyotokea

Jastus Juma majeruhi na Utingo wa Lori lililohusishwa na ajali hiyo amewaambia wanahabari kuwa Lori hilo halikuwa na matatizo yoyote na lilifanyiwa ukaguzi na maafisa wa polisi saa chache kabla ya kupata ajali.

“Dereva ainiambia kuwa breki haishiki nikajaribu kupiga kelele ili watu watoke barabarani kwenye kona pale watu hawakutoka ndipo tulipata ajali…gari haikuwa na tatizo lolote tatizo lilikuwa moja la gurudumu (tairi) ambalo tulirekebisha,” amesema Juma ambaye ni raia wa Kenya.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa anahojiwa na wanahabari jijini humo amesema Lori lilihohusishwa katika ajali hiyo lilikosa muelekeo kuanzia eneo la kilimamoto liliopo umbali wa kilomita nne mpaka ajali ilipotokea.

Naibu Waziri Dk. Godwin Mollel (kulia) akiwajulia hali majeruhi wa ajali katika Hospitali ya Mount Meru. Picha|Wizara ya Afya.

“Huyu jamaa (utingo) alikuwa anapiga kelele anaelezea tanua!  tanua! Gari yake imekosa breki haina honi wala nini, ilikuwa ni ‘complicated’ (ngumu) lakini tunamshukuru Mungu,” amesema shuhuda huyo.

Tayari viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini na Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel wamewasili katika eneo lilipotokea ajali hiyo na hospitalini ambapo majeruhi wanapata matibabu.

Akizungumza baada ya kuwajulia hali majeruhi hospitalini, Dk. Mollel amesema Serikali itagharamia matibabu kwa majeruhi wote waliolazwa katika Hospitali hiyo.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza Majeruhi wote wa ajali hii kupatiwa matibabu bila kulipa gharama zozote,” amesema Dk. Mollel.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW