Maelfu wajitokeza kumuaga Mwinyi Dar es Salaam, viongozi wamlilia
- Viongozi wajitokeza kutoa heshima zao za mwisho.
- Dk. Philip Mpango asema Mwinyi atakumbukwa kwa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.
Dar es Salaam. Mwili wa hayati Ali Hassan Mwinyi umeagwa jijini Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na maelfu ya wananchi wamejitokeza kumuaga kiongozi huyo atakayekumbukwa kwa mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi nchini.
Miongoni mwa viongozi waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyekuwa Rais wa Tanzania wa awamu ya pili kati ya mwaka 1985 hadi 1995 ni pamoja na Dk. Philip Mpango aliyesema Mwinyi alikuwa baba wa mageuzi.
Wengine ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mtoto wa marehemu, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, mawaziri, manaibu waziri na viongozi wengine wa Serikali.
Hayati Mwinyi aliaga dunia Februari 29 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam baada ya kuugua maradhi ya saratani ya mapafu tangu Novemba mwaka jana na anatarajiwa kuzikwa Machi 2 visiwani Zanzibar.
Kabla ya mwili huo kuagwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ulipitishwa katika barabara ya Morogoro kutoka nyumbani kwa kiongozi huyo Mikocheni kupitia Morocco na baadae katika Msikiti wa Ijumaa kwa ajili ya Swala.
Safari hiyo ya mwisho ya kiongozi huyo iliendelea hadi mwili ulipofikishwa katika uwanja Uhuru ambapo maelfu ya Watanzania walijitokeza kumuaga.
Viongozi wamemwelezea hayati Mwinyi kuwa alikuwa mtu asiyependa kujikweza na mwenye maamuzi magumu ambayo yamesaidia nchi kupiga hatua nchini.
Soma zaidi:Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia
Dk.Mpango amesema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa hayati Mwinyi alikuwa ni baba wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.
“Tunashukuru sana kwa zawadi ya maisha yake, tunathamini mchango na wake katika maendeleo Tanzania,” amesema Dk.Mpango.
Hayati Mwinyi wakati wa uongozi wake aliiongoza Tanzania katika mageuzi kutoka kwenye uchumi wa kijamii kwenda uchumi wa kiliberali jambo liliruhusu kustawi kwa sekta binafsi na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma.
Mwinyi pia atakumbukwa kuwa kiongozi aliyesimamia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kidemokrasia nchini baada kuchukua uamuzi wa kuanzisha vyama vingi baada ya Tanzania kuwa katika mfumo wa chama kimoja kwa miongo mitatu.
Katika hotuba yake wakati wa kuuaga mwili wa hayati Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema katika uongozi wake kulikuwa na vuguvugu la kuleta mabadiliko ya kisiasa ndani ya nchi na katika maeneo mengine duniani.
“Mzee Mwinyi aliunda tume ya Nyalali ikaleta mapendekezo (ya kuanzisha vyama), haikuwa rahisi kufikia uamuzi ni mabadiliko ya aina gani. Lakini chini ya uongozi wa Mzee Mwinyi, mageuzi yalifanywa. Na wakati wote ule mageuzi yalikuwa yanafanywa kwa kuzingatia kwamba tusije tukahatarisha umoja wetu, mshikamano wetu na amani yetu,” amesema Warioba.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mama Mary Majaliwa wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu wa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi.Picha|Ofisi yaWazir Mkuu.
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliwaeleza waombolezaji kuwa Mwinyi alikuwa kiongozi asiyependa makuu akithamini hata kundi dogo katika ufanyaji wa maamuzi ya kisiasa na kiuchumi.
“Katika mageuzi ya kisiasa iliundwa tume ya Nyalali iliyokuja na mapendekezo asilimia 80 wanasema tubaki na mfumo wa chama kimoja 20 wanasema tubaki na mfumo wa vyama vingi chini ya uongozi wake uamuzi ukafanyika wachache wape…hoja ikaja kwamba 20 siyo kidogo,” amesema Kikwete.
Baada ya mwili kuagwa kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam Saa 11 jioni, mwili wa kiongozi huyo umeelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Zanzibar na kufuatiwa na shughuli ya mazishi ya kitaifa kesho Machi 2, 2024.
Baadhi ya wananchi nao walipata fursa ya kuuga mwili wakati ukipitishwa bararabani wakiupungia mikono kuelekea uwanja wa ndege.
Latest
