Rais Samia aongoza maelfu kumuaga Mwinyi Zanzibar
- Awataka wananchi kumuenzi kwa kuendeleza uwajibikaji.
- Viongozi wa kitaifa kimataifa wajitokeza kumuaga.
- Amezikwa katika eneo la Mangapwani Unguja.
Dar es Salaam.Rais Samia Suluhu hassan ameongoza mamia ya Watanzania kuaga mwili wa Ali Hassan Mwinyi katika uwanja wa Amaan Zanzibar huku akiwataka viongozi na wananchi kumuenzi kwa kuendeleza uwajibikaji.
Mwili wa kiongozi huyo umeagwa leo Machi 2, 2024 kwa mara ya mwisho katika Uwanja wa Amani Zanzibar ikiwa zimepita siku mbili tangu kiongozi huyo apoteze maisha Februari 29 mwaka huu kwa maradhi ya mapafu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Saa 4:21 asubuhii mwili wa kiongozi huyo uliwasili katika uwanja wa Amani, Zanzibar kwa ajili ya kuagwa mara mwisho ambapo ulibebwa na kubebwa na wanajeshi waliokwenda kwa mwendo pole kama ilivyokawaida ya msiba ya Serikali hadieneo maalum lililoandaliwa.
Kabla ya Shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Mwinyi wanafamilia na viongozi mbalimbali walipewa nafasi ya kuwasilisha salamu za pole na rambi rambi kwa Watanzania na Rais wa Jamhuri ya Tanzania.
Soma zaidi:Maelfu wajitokeza kumuaga Mwinyi Dar es Salaam, viongozi wamlilia
Akizungumza katika safari hiyo ya mwisho ya hayati Mwinyi anayetajwa kuwa muasisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa nchini Tanzania, Rais Samia amesema kiongozi huyo alikuwa hodari na jasiri atakayekumbukwa ndani na nje ya nchi.
“Hatuna budi kumuenzi mzee wetu kwa kuiishi dhana ya uwajibikaji kwa mapana hayo…Afrika Mashariki itamkumbuka kwa kuwa mmoja wa waasisi wa kufufuliwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Afrika kwa ujumla itamkumbuka,” amesema Rais Samia leo Machi 2, 2024.
Naye Rais Mstaafu wa awamu ya sita Zanzibar Dk.Amani abeid Karume, amewataka viongozi waliopo madarakani kuuenzi wosia wa hayati Mwinyi kwa kuwa waadilifu na kufanya usuluhishi.
“Ombi Langu kwenu viongozi na tunaoongozwa tuendeleze kazi ya kusuluhisha nyoyo za wananchi wetu na hiyo ndio kazi yetu ya kila siku,” amesema Dk. Karume.
Kwa upande wake Dk.Mohamed Shain, aliyekuwa Rais wa awamu ya saba Zanzibar amesema Mwinyi atakumbukwa kwa uzalendo alioonesha katika Taifa lake hususani katika Sekta ya elimu aliyoisimamia vilivyo wakati akiwa mwalimu.
Baadhi ya wanafamilia wa hayati Ali Mwinyi wakiwa katika uwanja wa AmaniZanzibar kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao ambaye pia alikuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili.Picha|Ikulu
Safari ya mwisho wa kiongozi huyo pia imesindikizwa na viongozi kutoka nje ya nchi akiwemo Waziri wa Kilimo Comoro Houmed Msaidie aliyeeleza mchango wa Jina la ‘Mzee wa ruksa’ katika Taifa lake.
“Hili neno la Mzee wa ruksa hata Wacomoro wanalifahamu kwamba ni falsafa ya kusema kweli, Serikali fanyeni kazi zenu muamini vilevile wananchi wanalo jukumu la kukuza uchumi,” amesema Msaidie.
Viongozi wengine wa kimataifa waliohudhuria katika safari ya mwisho ya kiongozi huyo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah na Spika wa Bunge la Burundi Emmanuel Sinzohagera.
Baada ya kuagwa katika viwanja vya amani mwili wa Hayati umepelekwa katika msikiti wa Jamii Zanzibar kwa ajili ya swala kabla ya kwenda kuzikwa katika eneo la Manga pwani Unguja.