Si kweli: Watu saba wapofuka macho kisa ‘Red Eyes’
- Serikali yasema vyombo vya habari vimepotosha taarifa yake.
- Yasema matumizi ya tiba isiyo sahihi ya ugonjwa huo ndio yanaweza kusababisha upofu.
- Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara.
Dar es Salaam. Huenda ukawa miongoni mwa watu waliokutana na taarifa inayoenea katika mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram na X kuwa watu saba wamepofuka macho baada ya kujaribu kujitibu ugonjwa wa red eyes, fahamu kuwa siyo kweli.
Taarifa hizo zinanukuu chanzo chake kuwa ni Wizara ya Afya nchini Tanzania ambayo nayo imesema taarifa hizo siyo za kweli.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Engliberth Kayombo, amesema ni kweli Februari 6, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo alinukuliwa akisema wizara imeanza kupokea taarifa za watu ambao wamefika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa na vidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho.
Vidonda hivyo walivyopata mara baada ya kutumia tiba zisizo rasmi kutibu ugonjwa wa ‘Red Eyes’ (Macho Mekundu) ikiwemo dawa zenye vichocheo vya “Steriods”.
Dawa zingine zisizo rasmi ni tangawizi, chai ya rangi iliyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yanatumika wakati wa janga la Uviko-19, maji ya chumvi na maziwa ya mama, tiba ambazo si sahihi.
Kwa mujibu wa Kayombo, Prof Ruggajo aliyekuwa akizungumza na wanahabari, hakutaja idadi rasmi ya ya watu waliopatwa na upofu kutokana ugonjwa wa Macho Mekundu kama ilivyotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari.
Badala yake alitoa tahadhari kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujitibu kiholela ambavyo vinaweza kusababisha athari zaidi ikiwemo kusababisha upofu.
“Taarifa hiyo aliyoitoa haikutaja idadi ya watu waliopatwa na upofu kutokana ugonjwa wa Macho Mekundu kama ilivyotolewa kwenye Vyombo vya Habari. Prof. Ruggajo alitoa tahadhari kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujitibu kiholela ambavyo vinaweza kusababisha athari zaidi ikiwemo kupelekea upofu.” amebainisha Kayombo.
Kayombo amesisitiza kuwa ni muhimu vyombo vya habari na wanahabari kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kutoa habari za ukweli kutoka kwenye vyanzo vilivyothibitishwa.
“Afya ni suala la msingi na linamgusa kila mmoja, taarifa zisizo za ukweli kuhusu huduma za afya, magonjwa na sekta ya afya kwa ujumla zinaweza sababisha madhara zaidi kuliko hata lengo la utoaji wa taarifa wenyewe endapo taarifa haitokuwa sahihi”, amesisitiza Kayombo.
Ugonjwa wa Red Eyes uliripotiwa kuwepo nchini Januari 2024, ambapo katika kipindi cha Disemba 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kuliripotiwa kuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hususan katika mkoa wa Dar es Salaam waliofikia 869.
Ugonjwa huo unaofahamika kwa jina la kitaalam la ‘Viral Conjunctivitis’ husababishwa na bakteria, virusi au mzio na husambazwa kwa njia ya hewa.
Soma zaidi: Unavyoweza kuepuka ugonjwa wa ‘red eyes’
Huathiri ngozi ya juu ya gololi la jicho ambapo dalili zake ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, kutoa machozi na kutoa tongotongo za njano.
Wananchi wanashauriwa kuwafika katika vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu pale wanapopata dalili za ugonjwa huo ingawa ugonjwa huo hukoma wenyewe baada ya siku 14 kupita.
Miongoni mwa njia za kujikinga na ugonjwa huo ni pamoja na usafi yaani kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kutoshika macho, kutoshikana mikono na watu au kunawa baada ya kushikana mikono
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanafafanua kuwa ugonjwa huu sio wa hatari kiasi cha kusababisha madhara mengine ya kiafya kama upofu.