YouTube yamwaga mabilioni kwa watumiaji wake

September 3, 2021 11:39 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Imetenga zaidi ya Tsh200 bilioni kwa ajili ya kufadhili watengeneza maudhui mtandaoni.
  • Watalipwa wanaotumia kipengele chake cha YouTube Shorts.
  • Mpunga huo utatolewa mwaka mzima kuanzia Agosti 2021.

Dar es Salaam. Kwa umaarufu wa mtandao wa YouTube ambao ni mashuhuli kwa kutazamia maudhui ya video na sauti, bila shaka jukwaa hilo siyo geni masikioni mwako.

Mtandao huo ambao una watumiaji zaidi ya bilioni 2 duniani ni kati ya mitandao ya kijamii ambayo pia kwa baadhi ni sehemu yao ya kupata kipato.

Wasanii wa muziki, kutengeneza filamu na watu wote wenye akaunti za watengeneza maudhui yaani “creators” wanaweza kuingiza mpunga kadiri wanavyopata wafuasi na video zao zinavyotazamwa.

Mwanzoni mwa mwaka huu, YouTube ilizindua kipengele cha “YouTube Shorts” kwenye mtandao huo ambacho kinamuwezesha mtu kurekodi video ya sekunde 60 kama ilivyo kwenye majukwaa mengine ikiwemo Instagram, TikiTok na SnapChat.

Licha ya kipengele hicho kujitwalia watumiaji wengi ndani ya muda mfupi kikichuana vikali na TikTok, baadhi ya watu wamekuwa wakihoji jinsi mtu anavyoweza kutengeneza fedha kama ilivyo kwenye maudhui ya kawaida ya YouTube.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya CNBC, Shorts inapata hadi watazamaji bilioni 3.5 kwa siku, mbele kidogo ya TikTok ambayo inapata watazamaji bilioni 1 kwa siku, takwimu za hadi  mwisho wa mwezi Agosti 2021.

Kupitia Shorts, mtu anaweza kutengeneza fedha pale video zake zinapowafikia watu wengi zaidi. Picha| The Verge.

Unavyoweza kutengeneza fedha

Baadhi ya wasanii wa muziki, filamu na video za maudhui ya kufundisha na ya burudani, wamefanikiwa kutumia video za kawaida kama chanzo cha kupata kipato. 

Takwimu kutoka gazeti la Style zinaonyesha, mtumia mtandao wa YouTube anayelipwa zaidi ni kijana mwenye miaka tisa, Ryan Kaji ambaye hupakia video za uchambuzi wa vitu vya kuchezea (toys).

Kaji analipwa hadi Dola za Marekani milioni 29.5 kwa mwaka sawa na Sh 68.4 bilioni huku uku akiwa na wafuasi milioni 41.7.

Njia nyingine ya kuingiza kipato ni hizi video za muda mfupi (Shorts) ambazo kwa mujibu wa Shirika la Habari la The Verge, mtu anaweza kuingiza hadi Sh23.2 milioni kwa mwezi.

Siku za hivi karibuni, mtandao wa YouTube ulitangaza kuweka bajeti ya Dola za Marekani milioni 100 (Tsh231 bilioni) kwa ajili  ya kuwalipa watengeneza maudhui watakaotengeneza video maalumu kwa ajili ya kipengele cha Shorts.

Kwa mujibu wa YouTube, malipo hayo yatazingatia wapi hadhira ya mtengeza maudhui ipo na kama anatengeneza maudhui mapya (original) yasiyokuwa na alama au nembo ya mitandao mingine kama TikTok na mengineyo.

Fedha hizo zimeanza kutolewa mwanzo wa mwezi Agosti hadi kipindi hicho hicho mwakani (2022).

Kwa sasa mpunga huo unatolewa kwa watengenza maudhui wa nchini India na Marekani, Youtube inangalia namna ya kusogeza fedha hizo kwenye nchi zingine.

Hatua ya Youtube ni muendelezo wa ushindani baina yake na TikTok kwani mtandao huo nao ulitoa mpunga kwa watengeneza maudhui wake kama njia ya kuongeza motisha kwa watumiaji wake.

Duru za mitandaoni zinasema, TikTok imeweka bajeti ya Dola za Marekani milioni 200 (Sh463.7 bilioni) kwa ajili ya kuwafadhili watengeneza maudhui ya mtandao huo.

Kama wewe ni mtumiaji wa YouTube, changamka, huenda ikawa ni nafasi yako kutoboa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW