Vijana wanavyojiingizia kipato kupitia mtandao wa Tiktok
- Fedha hizo huwawezesha vijana kumudu gharama za maisha.
- Watumiaji wake hujiingizia kipato kupitia maudhui yanayohusu kupitia burudani, uhamasishaji na zawadi za moja kwa moja ukiwa mubashara.
Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii si jukwaa la kuunganisha watu na kutengeneza marafiki wapya tu, ila inaweza kugeuka mgodi wa dhahabu muda na saa yoyote ukiamua hususan ukiwa na vitendea kazi muhimu kama simu na ‘bando’.
Miongoni mwa mitandao maarufu ambayo inaweza kugeuka fursa kwa vijana kujiingizia kipato ni pamoja na Tikok, YouTube, X, Snapchat, Facebook ambayo tafiti iliyofanywa na Shirika la Data la DataReportal inaitaja kutumiwa na idadi kubwa ya watu duniani.
Si hivyo tu, mitandao hiyo kwa sasa inawaingizia pesa zaidi ya asilimia 96 ya watengeneza maudhui duniani jambo linalochochea kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Miongoni ya watengeneza maudhui hao wanaonufaika na mitandao ya kijamii ni Flora Francis (22) mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayetumia mtandao wa Tiktok kujiingizia kipato kila mwezi.
Flora ameiambia Nukta habari kuwa anajipatia wastani wa zaidi ya Sh 300,000 kila mwezi kupitia video za burudani, uhamasishaji na zawadi za moja kwa moja kutoka kwa mashabiki zake wakati anapokuwa mubashara (live) kupitia mtandao huo.
“Nilianza kwa lengo la kujifurahisha kama wengi wanavyofanya lakini imekuja kubadili mtazamo wangu baada ya kuona naweza kuingiza pesa.” ameeleza Flora.
Flora alianza safari yake ya kutumia Tiktok mwaka 2023 akiwa na lengo la kujifurahisha tu kama ilivyo malengo ya watumiaji wengi wa mitandao hiyo lakini hivi sasa ana wafusi takriban elfu sita wanaomuwezesha kujiingizia kipato hicho.
Hata hivyo, safari yake haikuwa rahisi. Flora anakiri kwamba amekutana na na changamoto kama vile maneno ya kashfa kutoka kwa watu wa mtandaoni na shinikizo la kushindana na wabunifu wengine.
Aidha Flora ametoa ushauri kwa vijana wa Tanzania ambao hawana mchongo wowote na wanatumia mitandao ya kijamii kuitumia kama fursa ili kujiingizia kipato na sio kufanya maudhui yasiyokuwa na tija kwa lengo la kujifurahisha tu.
“Watu wanatenegeneza kiasi kingi sana cha pesa, kama ukiwa makini na unachokifanya” alimaliza Flora.
Si Flora pekee anayenufaika na mtandao huo, Abdul Mahmud (19 ) mkazi wa Arusha anakiri jinsi mtandao huo unavyomuingizia pesa zinazomsadia kujikimu kwa matumizi yake binafsi.
“Nimeanza kuingiza pesa kuanzia mwezi Aprili mwaka huu na kwa mara ya kwanza niliweza kutoa kiasi cha Sh 150,000,” amesema Abdul.
Abdul mwenye zaidi ya wafuasi 160,000 katika mtandao wa Tiktok, ameeleza kuwa pesa hizo anazipata zaidi kupitia (live) ambapo hupata zawadi za moja kwa moja kutoka kwa mashabiki zake huku kiasi kidogo kupitia ‘Promotion’.
Aidha, Abdul ameeleza kuwa ukiacha kuingiza pesa mtandao huo wa Tiktok ambao unapigwa vita katika mataifa mengi tofauti umeweza kumuongezea kujiamini na kupata marafiki wapya kwani mtandao huo umemuwezesha kutambua kipaji chake cha uchekeshaji.
Jinsi ya kujiingizia kipato Tiktok
Mbali na kitovu cha burudani mtandao wa Tiktok hutoa njia kadhaa za kupata mapato hususan kupitia Mfuko wa Watengeneza Maudhui (Creator Fund) ambao huwalipa wabunifu wanaokidhi vigezo kwa maudhui maarufu kulingana na idadi ya watazamaji na ushirikiano wa hadhira.
Ikiwa unahitaji kuanza kupokea ‘maokoto’ kupitia mtandao wa Tiktok ni lazima uzingatie vigezo kadhaa ikiwemo kutimiza mahitaji ya kijiografia yaani kuishi katika nchi amabazo Tiktok wamewezesha watengeneza maudhui kulipwa, mfano Tanzania.
Kigezo kingine ni kuwa na akaunti ya Tiktok, kupakia video zinazozingatia miongozo ya jumuiya ya Tiktok (Tiktok Community Guidelines) kuwa na wafuasi wasiopungua 10,000 na kupata angalau maoni 100,000 kwenye Tiktoks ulizochapisha ndani ya siku 30.
Ukishahakikisha kuwa umekidhi vigezo, unaweza kujisajili kwa kubonyeza kitufe cha ‘Creators tool’, na Tiktok itaanza kuhesabu malipo moja kwa moja kwa kuzingatia vipengele vya maudhui yako.
Hakuna kiwango maalumu na huenda usipate kipato kikubwa kama cha Influencers, lakini bado ni njia nzuri ya kujiongezea pesa za ziada, kwasababu Tiktok hulipa kutokana na utendaji wa akaunti yako.
Pia Tiktok ina ‘Creator Marketplace’ ambayo inaunganisha chapa na influencers kwa ushirikiano wa kulipwa pamoja na kuruhusu watumiaji kupata mapato kupitia zawadi za moja kwa moja na vidokezo vya kidijitali wakati wa live streaming (hii ni kwa watu waliofikisha wafuasi kuanzia 1,000 tu) ikiwaruhusu mashabiki kuwasaidia wabunifu moja kwa moja.