Jinsi ya kudhibiti hasira
- Ni pamoja na kuzijua dalili za hasira kupanda.
- Pia kujifunza kufikiria kabla ya kutenda.
- Unapona hasira zinaanza kupanda, fikiria njia za amani za kutatua changamoto.
Dar es Salaam. Ni jambo gani linaweza kukusababisha hasira zako zipande?
Kwa wengine ni kutukanwa, wengine ni maudhi madogo madogo na wengine ni matarajio yao kutokutimia.
Tatizo siyo kuwa na hasira, bali ni yale unayoweza kuyafanya ukiwa na hasira. Wapo ambao hujikuta wakifanya maamuzi magumu wanayoishia kuyajutia baadaye na wengine husema maneno wasiyoyamaanisha kwa watu.
Ili kuepukana na hali hiyo, zipo njia za kudhibiti hasira zako ili kuondoa majuto ambayo hayatokusaidia chochote bali kuharibu mahusiano usiyoweza kuyarudisha kwenye hali ya zamani.
Fikiria kabla ya kunena na kutenda
Inaweza kuwa ngumu kwani tayari volkano ya hasira yako inaweza kuwa imeanza kutokota lakini muda upo kabla haujaamua kufungua kinywa chako au kukunja ngumi zako kuyaunda majuto.
Chukua muda wa kupandisha na kushusha pumzi huku ukiwaza matokeo ya hasira zako na kama upo tayari kuyakabili.
Itakuepushia na gharama za matibabu pale utakapoumia au kuumiza mtu lakini pia kukutunzia muda ambao ungeutumia kwa kuomba radhi kwa mtu ambaye umemnenea maneno usiyomaanisha.
Fahamu kuwa hasira zako zitamuathiri mtu mwingine hivyo ni heri kutumia busara. Picha| Outreach Magazine.
Jaribu njia za amani
Pale kibiriti cha hasira zako kinapotikiswa, unaweza kutafuta njia za amani za kutatua changamoto iliyopo mbele yako. Zipo nyingi.
Unaweza kuchagua kuondoka kwenye eneo hilo kabla hasira zako hazijaripuka, ukaenda sehemu nyingine kupoa. Au unaweza kuchagua kumwambia anayekukosea kwa utaratibu kuwa haupendi anachokifanya.
Tovuti ya Mayo Clinic inayoandika juu ya masuala ya afya imeeleza kuwa, dakika chache za utulivu zinaweza kukusaidia kushusha hasira zako. Unapohisi zinaanza kutokota, jitenge na eneo linalokupa hasira hizo.
Jifunze mbinu za “kurelax”
Tovuti ya masuala ya kiafya, Healthline inashauri kuzifahamu mbinu ambazo hushusha hasira zako chini. Kwa wengine ni kula chakula kizuri, wengine kufanya mazoezi na wengine kusikiliza muziki.
Chagua na ijue mbinu yako ili hasira zako zinapoanza kupanda iwe rahisi kuzikandamiza lakini pia utafute pa kuzitolea.
Wapo ambao huenda kuzitolea hasira zao kwenye nyumba za kufanyia mazoezi maarufu kama “gym” kwa kufanya mazoezi, wengine huenda ufukweni na kupiga kelele na wengine huvunja vitu. Chagua njia yako.
Haitokusaidia chochote kufanya maamuzi ukiwa na hasira. Picha| Everypixel.
Vijue viashiria vyako
Kila mtu na dalili zake za hasira. Wapo wanaouma meno, wengine hutokwa na jasho jingi, kutetemeka, sauti kupanda na moyo kudunda kwa utofauti.
Tovuti ya Reach Out imeeleza, ukiijua dalili yako itakuwa rahisi kuwaambia hata rafiki zako wakuzuie pale wanapoanza kuziona dalili za hasira zako kupanda endapo wewe ni ngumu kujizuia.
Muhimu kuwa mkweli kwa watu wanaokuzunguka ili wasitikise kiberiti cha hasira zako na wajue cha kufanya pale mori zinapopanda.
“Homework” yako hii hapa
Haijalishi wewe ni mpole kiasi gani, lazima kuna kitu ambacho kikifanyika tofauti kinaweza kukufanya upoteze reli ya upole wako.
Ni muhimu kujichunguza na kufahamu kwani wapo watu ambao wana majuto hadi sasa kwa kudhindwa kuzizuia hasira zao. Jitafiti, jijue na ujidhibiti. Hasira Hasara!
Latest
