Machinga wakubali kwenda maeneo mapya ya biashara Mwanza
- Waondoka barabarani na kuhamia walikopangiwa na jiji.
- Waomba wajengewe miundmbinu ikiwemo vyoo.
- Serikali yasema ambao bado wafanye hivyo kwa hiari.
Mwanza. Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga jijini Mwanza wameanza kuondoka katika maeneo yao waliyokuwa wanafanyiabiashara awali ikiwemo kando ya barabara na kuhamia katika maeneo mapya waliyopangiwa.
Huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Septemba 13 mwaka huu aliagiza wamachinga wapangwe upya kwa kutafutiwa maeneo ya kufanyia biashara ili kuondoa usumbufu barabarani.
Nukta habari (www.nukta.co.tz) leo Oktoba 12 imeshuhudia wafanyabiashara waliokuwa wanafanyia biashara zao eneo la Makoroboi wakihamisha bidhaa zao na kwenda katika uwanja wa Mchafukuoga, Mtaa wa Igogo ambako Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilielekeza wahamie.
Wafanyabiashara wengine waliokuwa wanafanyia biashara zao katika mzunguko wa mnara wa saa (roundabout) nao wameelekea katika viwanja vya Mbungani ambako awali walipangiwa kwenda.
Hivi karibuni gari la matangazo lilipita katika kila kona ya jiji la Mwanza likiwataka wafanyabiashara kuondoa bidhaa zao katika njia za waenda kwa miguu na pembezoni mwa barabara na mitaro kuhamishia biashara hizo katika maeneo yaliyoelekezwa.
Mfanyabiashara, Hilda Amosi amesema wanaondoka kwenye maeneo yao ili kutii agizo lililotolewa na mkurugenzi wa jiji hilo lililowataka wahamie katika maeneo yaliyopangwa.
“Tunaomba machinga wote ambao bado wapo kwenye maeneo ya mzunguko wa Nyerere na wengine waondoke warudi huku kwa kuwa hao ndiyo sababu ya wateja kutofika kwenye maeneo haya na kwamba bidhaa tunazouza huku ndiyo wanauza huko pia,” amesema Hilda ambaye anafanyia biashara Mbugani.
Kuondoka kwa wafanyabiashara katika maeneo hayo kutasaidia kupunguza misongamano na usumbufu hasa kwa watembea kwa miguu na kupunguza uchafuzi wa mazingira hasa pembezoni mwa barabara.
Mwenyekiti wa soko Kuu jijini Mwanza, Ahmed Nchora amesema hadi sasa zaidi ya machinga 800 waliokuwa wameacha vizimba vyao sokoni hapo na kuhamishia bidhaa zao barabarani wamerudi katika maeneo yao ya zamani.
Amesema kamati ya usimamizi ya jiji la Mwanza imewasaidia wafanyabiashara hao kuhamia katika maeneo hayo ambapo watatakiwa kulipia gharama ya kizimba ya Sh3,000 pamoja na gharama zingine za usafi na leseni.
“Hapa katikati ya jiji tulikuwa na masoko mawili ya Mbugani katika eneo hilo kulikuwa na vitengo tofauti tofauti. Mfano kulikuwa na kitengo cha Mkunguni ambapo kulikuwa na vizimba 121 lakini walihama wote wakabakia wawili hivi sasa wote wamerejea,” amesema Nchora
Eneo lingine ndani ya soko hilo ni Chakaranga lililokuwa na vizimba 156 ambapo walibaki wafanyabaishara 30 lakini toka zoezi lianze wafanyabiashara wote wamerudi.
Baadhi ya wafanyabiashara jijini Mwanza wamehamisha biashara zao kutoka barabarani na kwenda katika maeneo waliyopangiwa. Picha| Mwananchi.
Hatua zaidi
Amesema ndani ya jiji la Mwanza lina jumla ya masoko 14 lakini wafanyabiashara waliyakambia na kuhamishia bidhaa zao barabarani kitendo ambacho ni hatari na kuwataka wafanyabiashara ambao bado hawajahamia katika maeneo mapya wafanye hivyo.
“Niwaombe wafanyabiashara waingie masokoni, masoko mengi yalikuwa wazi wafanyabiashara waliyakimbia hivyo warudi tufanye biashara. Kufanya biashara barabarani ni kujitafutia hatari,” amesema Nchora
Mwenyekiti huyo pia ameiomba Serikali kuanzisha stendi za daladala katika maeneo ya masoko ili kupunguza usumbufu wa wafanyabiashara hao pindi wanapotoka kuhemea mizigo yao.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma) mkoani Mwanza, Said Tembo ameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ikiwemo kuweka vyoo na huduma za maji katika maeneo ambayo wafanyabiashara wamepangiwa.
“Hakuna machinga ambaye anagoma kuondoka katika maeneo hatarishi na yasiyo rasmi, kinacholeta kigugumizi ni hofu ya baadhi yetu kama maeneo tunayohamishiwa yatakuwa na wateja wa kutosha wa bidhaa zetu,” amesema Tembo.
Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Seleman Sekiete amewataka machinga wote kuondoa biashara zao kwenye maeneo ya waenda kwa miguu na kuende katika maeneo waliyopangwa.
Sekiete amesema tayari taratibu zote za kuwahamisha machinga zimekamilika hivyo waende bila kusukumwa.
Latest