Kamati yaundwa kudhibiti wanyama wanaosababisha ajali viwanja vya ndege Tanzania
- Ni wanyama na ndege hai ambao huingilia shughuli za viwanja vya ndege.
- Wanyama husababisha ajali za ndege.
- Serikali yaunda kamati kutafiti suala hilo nchini nzima.
Mwanza. Serikali imezindua kamati ya kitaifa itakayojihusisha na kudhibiti wanyama na ndege hai wakiwemo kunguru na mwewe ili kupunguza matukio ya ajali katika viwanja vya viwanja vya ndege nchini Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel aliyekuwa akizungumza baada ya kuzindua kamati hiyo Oktoba 22, 2021 amesema kamati hiyo itasaidia katika kufanya utafiti na kuainisha tatizo na namna ya kulitatua ili kupunguza ajali zinazosababishwa na viumbe hao.
“Kamati imezinduliwa wakati mwafaka ambapo shirika la ndege nchini limeimarika, hivyo itasaidia katika kubaini tatizo na kuja na mapendekezo yatakayosaidia katika kudhibiti viumbe hao na kuimarisha usalama katika masuala ya anga,” amesema Gabriel.
Kwa mujibu wa Mhandisi Gabriel, tafiti zilizofanywa katika maeneo mbalimbali duniani zinabainisha kuwa katika kila miruko 10,000 ya ndege, asilimia tatu ya miruko hiyo hutokea ajali zinazosababishwa na viumbe hao.
Kamati hiyo ya Kitaifa itazunguka katika viwanja vyote nchini kufahamu hali halisi ya matukio hayo ya wanyama na kutafuta suluhu za kudumu ili kuhakikisha safari za anga zinakuwa salama kwa watumiaji wake.
“Tumebaini kuwa viumbe hai hao wasipodhibitiwa wanaweza kusababisha shida na tatizo hilo ni kubwa kidunia na linasababisha ajali nyingi,” amesema Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Paul Rwegasha.
Meneja wa Uwanja wa ndege, Pascal Karumbe akizungumza na kamati ya kitaifa ya udhibiti wa viumbe hai na wanyama wakati ilipotembelea kwenye kiwanja cha ndege cha Mwanza muda mchache baada ya Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel kuizindua. Picha na Mariam John.
Hatua zilizochukuliwa
Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mwanza, Paschal Karumbete amesema katika kipindi cha miaka mitano toka mwaka 2017 hadi mwaka huu jumla ya matukio 65 ya wanyama yametokea katika uwanja huo.
Amesema ndege aina ya mwewe ndiyo wanaoongoza kuruka kwenye eneo hilo.
“Kutokana na changamoto tumeweka watu 28 ambao hufanya kazi ya kulinda na kufukuza viumbe hao katika eneo hili, watu hawa pia hutusaidia kufanya utafiti kubaini viumbe hao hufuata nini, je ni mizoga au maji kwa kuwa katika kiwanja hiki kuna mitalo mingi ya maji,” amesema Karumbete
Meneja huyo ameleeza katika uwanja huo asilimia 59 ya matukio hayo hutokea wakati ndege ikiwa iko mita 30 kushuka chini, huku asilimia 92 hutokea wakati ndege ikiwa mita 900 na ni nje ya uwanja.
Anasema kinachofanyika ni kutoa elimu kwa wananchi hususani wafugaji kwa kuwa uwanja huo umezungukwa na shughuli nyingi za kibinadamu ikiwemo uvuvi, masoko na wakulima .
Pia hukata miti iliyo karibu na eneo hilo licha ya kuwa uwanja huo pia una changamoto ya kuzungukwa na milima ambapo viumbe hao huishi humo.