Vita dhidi ya visumbufu mazao, mimea inavyopiganwa Tanzania

May 9, 2023 5:12 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali itanunua viuatilifu lita 101,000 kukabiliana na visumbufu mazao.
  • Itaimarisha kilimo anga kwa kununua ndege.
  • Hiyo itasaidia kuongeza tija na kuimarisha sekta ya kilimo nchini. 

Dar es Salaam. Serikali imesema katika mwaka wa fedha wa 2023/24 inatarajia kununua viuatilifu lita 101,000 na kuimarisha kilimo anga ili kukabiliana na visumbufu mazao na mimea wakiwemo nzige.

Visumbufu vingine ambavyo vitadhivitiwa mwaka ujao unaoanza Julai 1 mwaka huu ni  viwavijeshi, kweleakwelea, nzi wa matunda na panya ambavyo vimekuwa vikiharibu mazao na kuwaachia wakulima hasara.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali itasavei na kuainisha maeneo ya mazalia ya visumbufu vya mazao na mimea na kudhibiti visumbufu; itaimarisha udhibiti wa ubora wa viuatilifu vinavyozalishwa nchini na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi. 

“Kadhalika, itatoa mafunzo ya matumizi bora na sahihi ya viuatilifu,” amesema Bashe leo Mei 8, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 ambapo vita ya visumbufu hivyo itaongozwa na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA).

Wizara imenunua magari 10 na pikipiki 19 kwa ajili ya kuwezesha kufanya savei ya uwepo wa visumbufu hivyo katika maeneo mbalimbali ya nchi ili viweze kudhibitiwa kabla havijaleta madhara na kufanya uharibifu wa mazao. 

Kwa sasa, TPHPA inakamilisha ujenzi wa maabara ya kitaifa eneo la Mtumba mkoani Dodoma na maabara 14 katika mipaka katika vituo vya ukaguzi. 

“Maabara hizo zitatumika kwa ajili ya uchunguzi wa visumbufu na magonjwa ya mimea pamoja na ubora wa viuatilifu na masalia ya viuatilifu kwenye mazao na bidhaa za kilimo,” amesisitiza Bashe. 

Dawa ya wadudu inaweza kuwa sumu kwa afya ya binadamu, lakini jinsi dawa ya wadudu ilivyo hatari inategemea na utendaji wake. Picha | FSS.

Kilimo anga ni silaha nyingine

Wizara ya Kilimo imeendelea kuimarisha kituo cha Kilimo Anga kwa kukamilisha matengenezo ya ndege na taratibu za ununuzi wa ndege mpya moja ili kuondokana na utegemezi wa ndege za nje kwa ajili ya udhibiti wa visumbufu vya mazao. 

“Hadi Aprili, 2023 Wizara imekamilisha matengenezo ya ndege ya kunyunyuzia viuatilifu iliyokuwa Nairobi nchini Kenya na taratibu za kuirejesha nchini zinaendelea,” amesema waziri huyo.

Pia manunuzi ya ndege mpya kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa visumbufu kwa njia ya anga yamefikia hatua ya tathmini ya kampuni tatu zilizoainishwa kwa ajili ya utengenezaji wa ndege maalum za udhibiti wa visumbufu. 

“Imefika wakati kama nchi kujitegemea katika udhibiti wa nzige, kweleakwelea na visumbufu vingine vya milipuko kwa kutumia ndege zetu za unyunyuziaji badala ya kuendelea kutegemea ndege za mashirika ya nje,” amesema Bashe. 


Soma zaidi:


Mapambano yanaendelea…

Mwaka 2022/23, Serikali ilipanga kununua lita 118,500 kwa ajili ya kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea lakini hkufikia Aprili, 2023 imenunua lita 106,000 sawa na asilimia 89.45 ya lengo.

Aidha, lita 82,124 za viuatilifu zimesambazwa katika Halmashauri 58 za mikoa ya Manyara, Singida, Tabora, Katavi, Tanga, Geita, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha na  Dodoma.

Viuatilifu hivyo vimesaidia kudhibiti milipuko ya viwavijeshi, nzi wa matunda na panya na kuweza kuokoa upotevu wa mazao ya mpunga, mahindi, mtama na uwele katika eneo la hekta 110,000 za mashamba ya wakulima. 

Pia mwaka huu wa fedha unaoisha Juni 30, Serikali  imedhibiti milipuko ya ndege waharibifu wa mazao (kwelea kwelea) katika Halmashauri 11 za mikoa ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Manyara na Singida ambapo lita 2,670 za viuatilifu zimetumika.

“Kilo 2,000 za viuatilifu zimetumika kudhibiti panya katika mikoa ya Morogoro, Mtwara na Lindi pamoja na lita 300 kwa ajili ya kudhibiti nzi wa matunda katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Mwanza,” amesema Bashe.  

Pia, TPHPA imenunua ndege zisizo na rubani (drones) 20 kwa ajili kuimarisha udhibiti wa visumbufu vya mimea. 

Vifaa vya kupimia vinasaba (portable DNA sequencer) 19 kwa ajili ya kutambua kwa urahisi wadudu, magonjwa na magugu vamizi kwenye mimea na mazao na aina ya mazao na bidhaa za kilimo zinazotoka na kuingia nchini kwa kuonyesha vinasaba vyake (DNA) vimenunuliwa. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...