Corona: Unawaji mikono ulivyosaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko Kanda ya Ziwa
- Wasaidia kubadili mila na desturi za watu kuhusu unawaji mikono.
- Imesaidia kupunguza magonjwa ya kuhara, kipindupindu na kichocho.
- Serikali yawasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Mwanza. “Magonjwa ya mlipuko mara nyingi yalijitokeza kipindi cha mvua, wakazi wanaoishi mwambao wa ziwa ndiyo waathirika zaidi kwa kuwa mara zote hutumia maji ya Ziwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya nyumbani,”
Ni kauli ya Benjamin Kisuka mkazi wa kijiji cha Kangunguli, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, ambacho ni miongoni mwa maeneo ya visiwani ambayo yalikuwa yakikumbwa na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara.
Magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakiwasumbua wakazi wa visiwani vilivyopo Ziwa Victoria ni pamoja na kuhara, kipindupindu na kichocho.
Wakazi wa kijiji hiki kilichopo umbali wa kilomita 20 kutoka mji wa Nansio, kwa sasa, wamepata ahueni baada ya magonjwa hayo kupungua kutokana msisitizo wa kampeni ya unawaji mikono.
Kampeni hiyo ilitiriwa mkazo tangu Machi 2020 mara baada ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) kuingia Tanzania. Unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni ni moja ya afua dhidi ya ugonjwa huo.
Tahadhari nyingine ni matumizi ya vitakasa mikono, uvaaji wa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuchanjwa chanjo ya Uviko-19.
Utekelezaji wa tahadhari hizo hasa unawaji mikono umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya Uviko-19 na magonjwa mengine ya mlipuko katika maeneo mbalimbali duniani.
Kisuka anasema yeye na familia yake kwa sasa hawaendi hospitali mara kwa mara kutibiwa magonjwa ya kuhara kwa sababu wanazingatia unawaji mikono na usafi wakiwa nyumbani.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Kangunguli, Sungulwa Mgema anasema kuwa miaka ya nyuma magonjwa ya mlipuko yalikuwa mengi lakini kwa sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu watu wameelimika na wanazingatia kanuni za usafi katika maeneo yao.
“Nina miaka sasa sisikii magonjwa hayo siyo kwamba hayapo lakini ni tofauti na miaka hii ambapo wengi wanajitahidi kufanya usafi, kuchemsha maji ya kunywa na kujisaidia kwenye vyoo,” anasema Sungulwa, mama wa mtoto mmoja.
Suala la kunawa mikono kwa maji tiririka katika maeneo mbalimbali ya nchi limekuwa jambo la kawaida kwa sasa hadi kwa watoto wadogo ambao ndiyo walikuwa wakisumbuliwa zaidi na magonjwa ya mlipuko.
Vifaa vya kunawia mikono kwa sasa vinapatikana katika maeneo mengi ikiwemo migahawa ili kutoa fursa kwa watu kusafisha mikono yao kabla na baada ya kupata huduma. Picha| Mariam John.
Kupungua kwa magonjwa ya mlipuko mara baada ya Uviko-19, pia kumeshuhudiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini hapa ambapo baadhi ya wananchi wanakiri kuwa kampeni ya kunawa mikono imesaidia kuwaepusha na magonjwa hayo.
“Kwa sasa watu wameelimika, wanafuata kanuni za afya, pia hii kampeni ya unawaji mikono imesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza magonjwa hayo,” anasema Mkazi wa mtaa wa Bugogwa katika manispaa hii iliyopo kando ya Ziwa Victoria, Constantine Luhari.
Magonjwa ya mlipuko husababishwa na ulaji wa vyakula na maji machafu hasa yaliyochanganyika na vimelea vya vinyesi vya binadamu na wanyama. Mara nyingi hutokea kwa kunywa maji yasiyochemshwa na kutozingatia kanuni za usafi ikiwemo kula bila kunawa mikono.
Hata wanaokwenda kutibiwa hospitali wapungua
Kaimu Mganga Mfawidhi katika kituo cha afya Kangunguli wilayani Ukerewe, Dk Paschal Peter anasema miaka ya nyuma katika kituo hicho walikuwa wanapokea wagonjwa kati ya 30 hadi 40 kwa mwezi wa magonjwa ya mlipuko hasa kuhara lakini sasa idadi ya wagonjwa imepungua na kufikia wagonjwa 10 tu kwa mwezi.
Dk Peter anasema msisitizo wa wataalam wa afya wa kunawa mikono umechangia kupungua kwa idadi ya watu wanaotibiwa magonjwa hayo.
Takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe zinaonyesha kuwa magonjwa hayo yamepungua. Katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2021 wagonjwa waliotibiwa magonjwa hayo walikuwa 6,652 kutoka 12,406 waliotibiwa mwaka 2020.
Idadi hiyo ya mwaka jana imepungua kutoka wagonjwa 16,421 waliotibiwa mwaka 2019.
Hata hivyo, Dk Peter anasema magonjwa hayo yanaweza kuisha kabisa ikiwa watu wataondokana na imani potofu na kujikita kuzingatia kwa umakini usafi wa maeneo wanayoishi na vyakula wanavyokula.
“Elimu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko bado haijatiliwa mkazo, bado jamii inaamini kuwa yanasababishwa na kurogwa hivyo wengi hukimbilia kwa waganga wa kienyeji,” anasema Dk Peter.
Baadhi ya mila na desturi ikiwemo kunawa mikono katika chombo kimoja zinapaswa kuepukwa ili kutoa hakikisho dhidi ya magonjwa hayo.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali
Matokeo mazuri ya kupungua kwa magonjwa ya mlipuko, yamechangiwa na elimu na hamasa iliyotolewa na viongozi kuwahimiza watu kunawa mikono na kuimarisha usafi katika maeneo yao ili kujikinga na Uviko-19.
“Changamoto iliyokuwepo ni watu kutumia maji machafu na mazingira kuwa machafu, kwa sasa Serikali na asasi za kiraia zimechangia kutoa elimu ya usafi wa mazingira hali iliyosababisha magonjwa kama hayo kupungua,” anasema Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugogwa katika Manispaa ya Ilemela, Jagani Gwanduye.
Gwanduye anasema katika mtaa huo yapo mashirika mengi yasiyo ya kiserikali ambayo yanasaidia kutoa elimu kwa wananchi pamoja misaada mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Baadhi ya wanawake wakiwa na watoto wao katika kituo cha afya Kangunguli wilayani Ukerewe ambapo wanakiri kuwa magonjwa ya mlipuko kwa watoto wao yamepungua. Picha| Mariam John.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Dk Getera Nyangi anasema katika kipindi cha miezi 12 iliyopita magonjwa ya kuhara, kuharisha damu na homa ya matumbo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Ametaja tabia ya watu kunawa mikono kwa maji tiririka yaliyotokana na kampeni ya unawaji mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 imesaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na magonjwa hayo.
“Ni kweli kabisa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita hatujapata wagonjwa wa kuhara na homa ya matumbo, takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa haya yameshuka ndani ya kipindi hiki na hakuna sababu nyingine zaidi ya unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni,” anasema Dk Nyangi.
Hata hivyo, amewatahadharisha wananchi kuendelea kuzingatia usafi ili kuondokana na changamoto za kiafya ikiwemo magonjwa hayo.
“Ni vema wananchi wakazingatia kinga kwa kuwa gharama za matibabu ni ghali hivyo waendelee kuchukua tahadhari,” anasema Dk Nyangi.
Afisa Afya wa Mkoa wa Mwanza, Fungo Masalu anasema licha ya kwamba hawajafanya tafiti kuona hali ilivyo kuhusu magonjwa ya mlipuko kwenye jamii lakini takwimu zao zinaonyesha yamepungua.
Anasema zipo sababu nyingi zilizosababisha kupungua kwa magonjwa hayo huenda watu wamepunguza kwenda hospitali kutibiwa kutokana na imani potofu juu ya Uviko-19 au ni kweli kwamba kampeni ya unawaji mikono imesaidia magonjwa hayo kupungua.
Anasema wanaendelea kulifuatilia suala hilo ili kujiridhisha na kutafuta suluhu ya kudumu ya magonjwa ya mlipuko ambayo huwatesa zaidi watoto wadogo.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest