Corona ilivyochangia kushuka muamko wa kuchangia damu Kanda ya Ziwa
- Baadhi ya watu walikuwa wanahofiwa kuambukizwa Uviko-19.
- Hali hiyo ilisababisha upungufu katika benki za damu.
- Pia vifo vya wajawazito na watoto viliongezeka.
Mwanza. Wakati dunia ikiendelea na mapambano dhidi ya janga la Corona, ugonjwa huo pia umeathiri shughuli za uchangiaji damu nchini Tanzania, jambo lililosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya damu na vifo vya watu hasa wajawazito.
Afisa Uhamasishaji wa damu salama kituo cha Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando, Rehema Mgendi amesema tangu janga la Uviko-19 liingie nchini mwaka jana, lilibadilisha upepo wa wachangiaji ambao wengi waliogopa wakiamini wanaweza kuambukizwa ugonjwa huo.
Mabadiliko hayo yalisababisha upungufu wa damu katika benki ya damu salama kanda ya Ziwa.
Upungufu huo mkubwa wa damu ulijitokeza katika hospitali zinazohitaji damu kwa wingi ikiwemo ya Bugando ambayo kwa siku hutumia uniti 40 za damu na hospitali za Sekou Toure na Butimba ambazo hutumia uniti kati ya 20 na 25 kwa siku.
Mgendi alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana Septemba 16, 2021 kuelekea kampeni ya kuchangia damu inayolenga kuwaokoa wajawazito ambao wamebainika kupoteza maisha kutokana na upungufu wa damu.
“Upungufu wa damu ulikuwa wa msimu mfano wakati janga linaingia nchini watu wengi waliogopa wakiamini wataambukizwa ugonjwa wa corona, lakini pia hata mwaka huu kwenye mwezi wa sita na wa saba hali ilibadilika na kusababisha vifo vingi hususan vya akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano,” amesema Mgendi.
Mtaalam huyo amesema kwa sasa ahueni imeanza kuonekana kwa sababu elimu inazidi kutolewa na watu wanapata uelewa hivyo wanajitokeza kuchangia japo si kwa kiwango kikubwa.
“Tiba ya damu ni damu yenyewe, na siku zote damu haitoshi, na kwamba duniani popote hatujawa na kiwanda cha damu, kwahiyo damu zote zinatoka kwa binadamu hivyo ni vyema jamii ikawa na uelewa wa kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wanaohitaji damu kama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wenye magonjwa sugu na wale wanaopata ajali,” amesema Mgendi.
Mmoja wa wananchi mkoani Mwanza akichangia damu katika kituo cha damu salama Bugando. Picha| Mariam John.
Mkuu wa kitengo cha uhamasishaji damu salama kanda ya Ziwa, Hilda Fidelis amesema asilimia 80 ya wachangia damu ni wanafunzi hususan wa sekondari na kuwa wanapohitimu masomo yao wachangiaji hupungua.
Kitengo cha damu salama kimeanzisha kampeni ya wiki moja ya kuchangia damu ambapo zaidi ya chupa 600 zinahitajika ili kufikia malengo ya mwaka ya kukusanya chupa 20,000.
“Changamoto tunayokutana nayo ni uelewa mdogo wa wachangia damu wapo wanaoamini wakichangia damu itaisha mwilini au damu itaongeza mara mbili ya ile waliyonayo hivyo kuwalazimu kuchangia mara kwa mara,” amesema Fidelis.
Fidelis amebainisha kuwa sifa za mchangia damu lazima awe mtu mzima mwenye umri kuanzia miaka 18 hadi 65, awe na afya njema, asiwe anatumia dozi na mwenye uzito kuanzia kilo 50.
“Kuchangia damu ni jukumu la watu wote ingawa changamoto iliyopo ni baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia hivyo jukumu kubwa kuwabebesha wanafunzi ambao nao wakihitimu wachangiaji wanakuwa wachache kwakuwa wanaobaki shuleni wengi hawajafikisha miaka 18,” anasema Fidelis.
Hatahivyo amesema katika hospitali zozote damu haiuzwi inatolewa bure na kwamba daktari yoyote atakayebainika kuuza damu kwa mgonjwa hatua za kisheria zitachukuliwa.
“Tunaenda kutafuta damu kwa wananchi wajitolee bure na hawatutozi gharama yoyote iweje mgonjwa hospitali atozwe hela?,” amehoji mtaalam huyo na kueleza kuwa ikitokea kwenye benki ya damu imepungua ndugu wa mgonjwa huwa wanatakiwa kujitolea damu zao.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
