Vipaumbele vitano bajeti kuu ya Serikali 2022-23
- Ni pamoja na masoko yanayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.
- Serikali imepanga kuwekeza katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini.
- Mwaka 2022/23, Serikali kukusanya na kutumia Sh39.4 trilioni.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiandaa mpango wa bajeti ya mwaka 2022/23, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amevitaja vipaumbele vitano ambavyo Serikali itaangazia ikiwemo kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma Tanzania.
Katika mwaka 2022/23, Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh39.4 trilioni ambayo ni juu kidogo ya bajeti ya mwaka 2021/22 ambayo ni Sh36.6 bilioni.
Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kufikia Sh28.5 trilioni sawa na asilimia 72.5 ya bajeti yote.
Dk Nchemba ametaja vipaumbele hivyo Oktoba 3, 2021 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2022/23.
Amesema bajeti ya mwaka 2022/23 itajikita katika kutekeleza vipaumbele vikuu vitano vitakavyosaidia kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Dhamira ya Serikali ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Picha| DW.
1. Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi
Kipaumbele hiki kinajumuisha miradi ambayo itajikita katika kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa, kuimarisha utulivu wa uchumi jumla pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Dk Nchemba amesema kuwa, eneo hili pia litaangazia kuimarisha tafiti na maendeleo pamoja na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje na kuendeleza miundombinu na huduma katika maeneo ya reli, barabara, madaraja, usafiri wa maji, usafiri wa anga, tehama, nishati, bandari na viwanja vya ndege.
2. Kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma
Katika kutilia mkazo kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inatarajia kuweka kipaumbele katika miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana kwa wingi nchini.
Eneo hili pia linajumuisha miradi na programu zinazolenga kuboresha sekta ya utalii, huduma za fedha na bima.
Kilimo ni sehemu ya maeneo ambayo serikali itayafanya kipaumbele. Picha| Jamii Forum.
3. Kukuza biashara na uwekezaji
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi amesema kuikuza sekta hiyo kutazingatia programu zitakazoimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko kikanda na kimataifa.
Serikali itaangazia kukuza masoko yatakayotoa fursa kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ikiwemo bidhaa na huduma zitokanazo na kilimo, viwanda na utalii.
Dk Nchemba amesema, “Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Blue Print).”
4. Kuchochea Maendeleo ya Watu
Serikali pia imepanga kuangazia katika utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya watu ikiwemo kuboresha elimu na mafunzo katika ngazi zote, afya na ustawi wa jamii pamoja na hifadhi ya jamii.
Dk Nchemba amesema serikali itazingatia sensa ya watu na makazi, huduma za maji na usafi wa mazingira hususan mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Jiji la Dodoma pamoja na mipango miji, nyumba na maendeleo ya makazi.
“Eneo hili linajumuisha kuimarisha mfumo wa sheria na taasisi za utoaji haki na usimamizi wa utawala bora, ulinzi na usalama na utulivu wa ndani na nje ya nchi, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ikiwemo kuimarisha utoaji haki pamoja na ukuzaji wa maadili.” Amesema Dk Nchemba.
Vilevile, Waziri huyo amesema serikali itaendelea na utekelezaji wa shughuli za kuhamishia makao makuu ya Serikali Jijini Dodoma ikiwemo awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi na miundombinu katika mji wa Serikali Mtumba.
Serikali itazingatia sensa ya watu na makazi, huduma za maji na usafi wa mazingira. Picha| Wakala wa Maendeleo ya Kimataifa nchini Marekani.
5. Kuendeleza Rasilimali Watu
Eneo lingine ambalo serikali itaweka kipaumbele ni programu na mikakati inayolenga kuendeleza ujuzi wa rasilimali watu nchini.
Kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwemo kuwawezesha vijana kujiajiri.
“Serikali itaendelea kutekeleza programu ya kukuza ujuzi nchini kwa kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kupitia Programu ya uanagenzi kwa vijana, kutoa mafunzo, kurasimisha na kutoa vyeti kwa vijana waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu wa elimu ya juu,” amesema Dk Nchemba.
Vilevile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.
Latest
