Faida za kampuni, mtu “kujibrand” upya

November 10, 2021 11:38 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inasaidia kupata wateja wapya na kuwashikiria wa zamani.
  • Ni mwanzo mpya wa kubadilisha mwelekeo wa kampuni.
  • Inaondoa makosa yaliyofanyika nyuma.

Dar es Salaam. Kumbukumbu inaanzia kipindi nikiwa mdogo, mtandao wa mawasiliano uliokuwa ukiitwa Buzz ulibadilishwa jinana kuitwa Tigo huku Celtel ikiwa Zain na baadaye kuwa Airtel hadi leo.

Nilijiuliza kwanini wanabadilisha majina? Hata hivyo  sikulitilia maanani sana na hivyo sikupata jibu.

Kwa umri wangu nilijua ni mchezo wa maigizo tu.

Ni hadi siku za hivi karibuni ambapo kampuni ya teknolojia ya Facebook ikijibadilisha jina na kujiita Meta ndipo ilinibidi nianze kufuatilia umuhimu wa kampuni kufanya hivyo.

Inaweza isiwe jina la kampuni, wengine huhuisha nembo na wengine rangi za utambuzi wa kampuni zao. Sababu za kampuni kujihuisha au lugha nyepesi ‘kujibrand’:

Kunasa umakini wa wateja

Kama mtoto nyumbani, anaweza kuwa na vitu vya kuchezea vingi tu lakini bado akaviona havimfai kwa kuwa ameshavizoea. Ndivyo iliyo katika biashara, pale biashara inapobaki vile vile kwa kipindi kirefu, watu wanaweza kuizoea na hivyo kuanza kutekwa na biashara mpya zinazoingia mjini.

Tovuti ya masuala ya masoko ya kidijitali ya T.E Digital imeandika, baadhi ya vipengele hupitwa na wakati. Mfano rangi, picha, nembo hivyo ukihitaji kampuni yako ienende na usasa, unashauriwa kujihuisha.

Kampuni mbalimbali kwa mwaka zimekuwa zikibadilisha nembo, vifungashio na hata rangi za kampuni. Hautokuwa wa kwanza.

Inaweza ikawa mtu, kamouni na hata taasisi. Picha| Laptrinhx.

Kubadilisha mwelekeo wa kampuni

Kampuni inaweza kuwa sokoni kwa muda mrefu na bila shaka ndani ya kipindi hicho ni mambo mengi yanaweza kuwa yamebadilika ikiwemo misimamo ya kampuni na hata malengo.

TE Digital inashauri kujihuisha ili kampuni iendane na kinachoendelea kwa sasa.

“Chukua muda kuisoma kampuni yako, mahitaji yake na nembo yake. Kujihuisha inaweza kuwa kazi ngumu lakini inaambatana na matunda mengi,” imeandika TE Digital.


Kubadili mtazamo wa kampuni kwa wateja

Huenda kampuni imeshatembeza jina lake kwenye tope. Inawezekana kuna miradi haikukamilika na hivyo kuacha maswali kwa watu au kuna mahala mambo hayakwenda kama yalivyopangwa.

Hali hiyo inaweza kuikosesha kampuni wateja na mtazamo wake kwenye jamii kuchafuliwa.

Mtaalamu wa masuala ya “branding” kwa makampuni na watu binafsi, Charles Nduku almaarufu kama Mr brand ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kujihuisha ni kuacha nyuma mabaya yote ya kampuni au mtu.

“Kuhuisha kampuni inamaanisha unajitangaza upya kwenye jamii,” amesema Mr Brand.

Kujihuisha pia ni kutangaza mwanzo mpya wa kampuni au mtu na pia kutangaza uongozi mpya. 

Hautokuwa wa kwanza kujihuisha kama kampuni, wengi wameshaanza| Picha| Turbologo.

Nani anayeweza kujihuisha?

Huenda unadhani ni kampuni, taasisi au mashirika pekee ndiyo yanaweza kufanya hivyo na kutengeneza majina mapya. Hapana, kujihuisha inaenda mbali zaidi na kumfikia hata mtu binafsi.

Kama wewe ni mdau wa sanaa, bila shaka umesikia kuhusu Puff Daddy kuwa Diddy, Snoop Lion kuwa Snoop Dogg na Dogo Aslay kuwa Aslay. 

Yote ni kuendana na wakati na kuyasahau yale ambayo huenda yalitokea nyuma.

Mr Brand amesema, iwe ni kampuni, mtu au taasisi, pale unapojihuisha haiishii kwenye jina pekee. Inaenda kwenye muonekano, tabia na hata sifa.

“Ukijihuisha tunatarajia uzoefu tofauti,” ameseama Mr Brand.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW