Tigo yabadilisha jina sasa kuitwa Yas
- Ni sehemu ya mkakati wa kuboresha uzoefu wa wateja, kuleta ubunifu, na kuendelea kushindana katika soko la kidijitali linalobadilika kwa haraka
- Huduma zake ikiwemo jukwaa la pesa mtandao zitabaki kama kawaida
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Tigo imebadilisha rasmi jina lake na sasa itajulikana kama Yas, hatua inayochukuliwa kama sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma na kuimarisha uhusiano na wateja wake.
Mabadiliko hayo yametangazwa leo Novemba 26, 2024, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.
Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliyekuwa akizungumza kwenye hafla hiyo ameeleza kuwa mabadiliko hayo kama hatua muhimu katika kuendana na mahitaji ya sasa ya kidijitali na ushindani wa soko la mawasiliano.
“Uzinduzi huu wa chapa mpya unadhihirisha hatua nyingine muhimu ikionyesha ukuaji, kubadilika, na mtazamo wa mbele ambao ni muhimu katika enzi ya kidijitali inayobadilika kwa kasi ya leo. Chapa mpya tunayoizindua leo itaonyesha mafanikio ambayo yanazidi viwango vya kawaida katika kujenga uchumi wa nchi na kusaidia wateja na watumiaji kufanikiwa katika enzi hii ya kidijitali.”
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, ‘rebranding’ hii inalenga kuimarisha huduma za kidijitali, kuleta ubunifu zaidi, na kuboresha uzoefu wa mteja. Kampuni hiyo imeahidi kuendelea kutoa huduma bora huku ikizindua bidhaa na huduma mpya zinazolenga kuwaunganisha Watanzania kwa urahisi na kasi zaidi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Jérôme Albou, amesema “Leo, maono haya ya kubadilika kuwa kitu kikubwa zaidi yanakusudia kufungua fursa za kidijitali na kifedha kwa Watanzania, kuboresha uzoefu wa wateja wetu, kuungana na vijana, na kuimarisha uvumbuzi.”
Wateja wa Tigo wamehakikishiwa kuwa huduma na bidhaa walizokuwa wakizitumia hazitaathirika na kwamba mabadiliko hayo ni ya jina tu. Kampuni pia imetangaza kuwa itaanza kampeni kubwa ya mawasiliano na elimu kwa umma ili kuhakikisha wateja wanazoea jina hilo jipya na kuelewa malengo yake.
Kwa upande wa tigo pesa hivi sasa itaitwa ‘Mixx by Yas’, mabadiliko ya jina hayataathiri akaunti za pesa mtandao, zote zitaendelea kuwa hai na kufanya kazi, salio na huduma zinaendelea ilivyo kawaida na hakuna atakaehitaji kufungua akaunti upya.
Mabadiliko haya yanakuja wakati ambapo sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inaendelea kushuhudia ushindani mkubwa, huku makampuni yakilazimika kuleta uvumbuzi wa huduma ili kuvutia wateja.
Yas ilianza kufanya kazi Tanzania 1994 ikijulikana kama mobitel, 2006 ilibadilisha jina lake na kuanza kutumia jina Tigo kama sehemu ya jitihada za kujiimarisha sokoni na kujitofautisha katika sekta ya mawasiliano.
Kampuni mama ya Yas inaitwa AXIAN Telecom, inatoa huduma za mawasiliano barani Afrika katika nchi tisa tofauti ikiwepo Tanzania sambamba na Madagascar, Comoro, DRC, Reunion, Mayotte, Senegal, Togo, Uganda.