Waandishi habari 488 wafungwa jela, 46 wauawa 2021
- Idadi ya wanahabari wanaofungwa inaongezeka huku wanaouawa inapungua.
- Duluma dhidi ya wanahabari wanawake nazo zaongezeka.
- Sababu kubwa ni kuongezeka kwa tawala za kidikteta duniani.
Dar es Salaaam. Shirika la Waandishi Habari Wasiokuwa na Mipaka – RSF limesema kwa sasa kuna waandishi wa habari 488 waliofungwa jela huku 46 wameuawa wakati wakitimiza majukumu yao.
Idadi hiyo ya wanahabari waliofungwa jela ni kubwa zaidi tangu shirika hilo lilipoanza kuorodhesha matukio hayo miaka 25 iliyopita.
Kati yao, 60 ni wanahabari wanawake huku China ikiongoza katika nchi zilizowafunga waandishi habari wengi ikiwa na wanahabari 127.
Aidha, shirika hilo limesema kuwa halijawahi kuona waandishi habari wa kike wakikamatwa kama ilivyo sasa, ambapo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka 2020.
RSF imesema idadi ya waandishi waliouawa mwaka huu ni 46 ikiwa ni ya chini mno tangu ilipoanza kutoa takwimu za kila mwaka.
“Hii ni kutokana na kutulia kwa kiasi fulani kwa mizozo katika eneo la Mashariki ya Kati,” limeeleza taarifa ya RSF iliyotolewa Desemba 17, 2021.
Shirika hilo linalopigania uhuru wa kujieleza na waandishi wa habari, limesema idadi ya waliokamatwa imeongezeka kwa asilimia 20 kwa mwaka uliopita kwa kiasi kikubwa kutokana na ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari nchini Myanmar, Belarus na Hong Kong.
“Idadi kubwa ya waandishi wa habari walio kizuizini kiholela ni kazi ya tawala tatu za kidikteta,” amesema Katibu Mkuu wa RSF, Christophe Deloire na kubainisha kuwa,
“Ni udhihirisho wa kuimarishwa kwa mamlaka ya kidikteta duniani kote, mlundikano wa migogoro na ukosefu wa mashaka yoyote kwa upande wa tawala hizi. Inaweza pia kuwa matokeo ya uhusiano mpya wa mamlaka ya kijiografia ambapo tawala za kimabavu hazikutwi na shinikizo la kutosha ili kuzuia ukandamizaji wao.”
Baadhi ya wanahabari waliofungwa ni pamoja na Ali Abulohom wa nchini Saudi Arabia na Pham Chi Dung nchini Vietnam ambapo wote wanatumikia kifungo cha miaka 15.
Soma zaidi:
Wakongwe nao ndani
Wanahabari wakongwe zaidi wanaozuiliwa ni Jimmy Lai (74) aliyeko Hong Kong na Kayvan Sami Behbahani nchini Iran ambaye ana miaka 73.
Mwandishi wa habari wa Ufaransa, Olivier Dubois ndiye mwanahabari pekee wa kigeni aliyetekwa mwaka huu. Amekuwa mateka nchini Mali tangu Aprili 8 mwaka huu.
RSF imegundua kuwa asilimia 65 ya waandishi wa habari waliouawa mwaka 2021 walilengwa kwa makusudi na kuondolewa.
Mexico na Afghanistan ndizo ndizo nchi zinaongoza kwa mauaji ya waandishi wa habari ambapo saba waliuawa Mexico na sita huko Afghanistan.
Yemen na India zinashika nafasi ya tatu, huku waandishi wa habari wanne wakiuawa katika kila nchi.
Tangu mwaka wa 1995, RSF imekuwa wakiandaa duru za kila mwaka za vurugu na dhuluma dhidi ya wanahabari kulingana na data sahihi zinazokusanywa kuanzia Januari hadi Desemba ya mwaka husika.
RSF imesema takwimu hizo za dhuluma dhidi ya waandishi wa habari zinasaidia kufahamu hali halisi na mikakati ya kuboresha uhuru wa kundi hilo muhimu kw maendeleo duniani.
Latest
