Usikubali maneno ya watu kukatisha ndoto zako
- Kwa kila hali, wanadamu lazima watasema.
- Hofu ya “watu watanionaje” ni chanzo cha ndoto za baadhi kuyayuka.
- Kabla ya kuwaza kufurahisha watu, jifunze kujifurahisha wewe kwanza.
Dar es Salaam. Anza kwa kufikiria, hadi sasa kuna vitu vingapi haujavifanya kwa sababu ya kuhofia “watanionaje”?
Kuna siku moja nilikutana na kichekesho. Kilikuwa kimeandikwa “wakati unahofia kufanya kazi unayohisi haina hadhi, hao unaowahofia usiku wanakuwa wamelala, wamekula, wameshiba huku wewe ukiwa kwenye lindi la mawazo ya kutokujua hata siku yako inaanzaje.”
Kwanini unahofia maneno ya watu?
Msaikolojia Michael Gervais kupitia chapisho la Havard Business Review ameandika kuwa, watu hutafuta kukubalika na jamii zao hivyo hufuata yale jamii imeyatenga kama mambo yanayokubalika.
Hofu ya kukosolewa, kuchukiwa na kutokukubalika imewafanya baadhi ya watu kushindwa kufuata ndoto zao na kubaki wakihangaika kila siku kutafuta “kibali” kutoka kwa watu ambao huenda wasiwapatie hata kilo moja ya unga pale watakapokosa fedha ya chakula.
Gervais anashauri kuwa, ili kuepukana na hali hiyo, unaweza kuanza kwa kujenga falsafa yako inayohusisha mambo unayoyaamini na kuyafuata.
Kwa kila hali, hatokosekana mtu wa kusema. Picha| The Mix.
Utajuaje kama una hofu ya maneno ya watu?
Kabla ya kuendelea fahamu kuwa hofu siyo ugonjwa. Ni hali ambayo mtu anakuwa nayo kutokana na mazingira aliyopo au anayokulia.
Inaenda sambamba na hali ya kujiona duni kuliko wengine na kutaka kuwa kama fulani. Mfano, kama mtoto anataka kuwa mcheza mpira baadaye, anaweza akawa na mtu ambaye anamtazamia. Siku mtu huyo atakaposema “huwezi kuwa mcheza mpira kama haupo Ulaya” huenda kauli hiyo ikamkata maini mtoto huyo. Ni mfano tu.
Dalili za kuwa maneno ya watu yanaathiri maamuzi yako kwa mujibu wa tovuti ya Psyche Central ni pamoja na kujibadilisha baada ya kukosolewa, kukosa au kushindwa kufuata misimamo yako au unaukata ulimi wako kama mawazo yako yanatofautiana na ya kila mtu.
Viashiria vingine ni pamoja na kutaka kila kitu kiwe sawa (perfectionist), amani yako kutegemea vibali vya wengine na kushindwa kusema “hapana” kila mara.
Soma zaidi
- Huyu ndiye mtu sahihi wa kuanzisha naye mahusiano
- Sababu za kusinzia kazini na jinsi ya kuzuia
- Wafanyabiashara wasota na soko liloungua miaka saba Dar
Unachokikosa kwa kusikiliza maneno ya watu
Furaha yako binafsi
Wakati ukiwa bize kufurahisha macho ya watu ambao huenda ndani ya dakika kadhaa watazisahau kabisa juhudi zako, jiulize kama wewe unafurahia unachokifanya.
Huenda umewekeza katika kuonekana unafanya kazi kwa bidii lakini kumbe kazi yako hauifurahii.
Kwa kutaka kuoneka wa hadhi fulani, unajikuta unafanya usichopenda. Mwisho wa siku unapokuwa kitandani usiku, umechoka, unaanza kuwaza kama usingizie kuumwa ili usiende kazini.
Niliwahi kuongea na kaka yangu ambaye amekuwa mshauri wangu mkubwa. Ni mwalimu wa rasilimali watu, Moses Samora. Alinitumia video yenye ujumbe wa kuwa, “zawadi kubwa unayoweza kujipatia ni kutafuta kitu ambacho una ujuzi nacho na kutafuta njia unayoweza kutengeneza maisha kupitia kitu hicho.
Kwa sababu ukifanya hivyo, kila siku itakuwa siku ya michezo kwako.”
Tafuta furaha yako kwanza, kuwafurahisha wengine hakukufikishi kwenye kaburi ukiwa na tabasamu.
Ukiruhusu mtazamo wa mtu uongoze furaha yako, hautokuwa na amani na maisha yako. Picha| iStock.
Hofu ya kukosea
Endapo unamkumbuka mwalimu wako wa fizikia, hebu rudi darasani wakati akifundisha kuhusu yule aliyegundua balbu. Thomas Edison aligundua balbu lakini haukuwa ugunduzi wa siku moja. Kabla ya taa hiyo kuwaka, alikosea na kukosea hadi alipofanikiwa. Na sasa, hadi wewe unanufaika na matokeo yake ambayo yalipitia makosa mengi tu.
Msaikolojia Leslie Becker-Phelps kupitia tovuti ya afya ya WebMd ameandika kuwa, tatizo la kujali kile watu wanasema linaanza na mtu kujali zaidi maneno ya watu kuliko thamani yake.
Uskani wa hisia zako
Unapoogopa kufanya kitu kwa sababu ya hofu ya kukosa kibali cha watu unazifungia hisia zako sahihi na halisi. Huenda unayafungia mafanikio yako pia.
Kufanya hivyo kwa namna fulani inafungia furaha yako na hivyo, hisia zako zinakuwa zinaendeshwa na macho ya jamii.
Macho hayo yaamue kuwa ni muda wa wewe kufurahi au umekosea hivyo uone aibu.
Amka, nenda ukawe unachotaka. Beba begi, kauze hayo marashi, beba beseni lako, kauze hayo matunda kaimbe kwenye hilo jukwaa.
Furaha yako ni wajibu wako lakini hakikisha upo salama.
Latest