Mvua, upepo wasimamisha usafiri wa vivuko Ziwa Victoria
- Ni vivuko vinavyofanya safari Kigongo-Busisi mkoani Mwanza.
- Serikali yasema hali itarejea kama kawaida mvua ikipungua.
Mwanza. Wasafiri wanaopita katika barabara ya Kigongo-Busisi inayokatiza Ziwa Victoria mkoani Mwanza wamelazimika kutumia muda mrefu kuvuka kwenye kivuko hicho huku sababu ikitajwa kuwa ni kuwepo kwa mawimbi makali ziwani yaliyosababisha vivuko viwili kutofanya kazi.
Eneo la Kigongo-Busisi kuna vivuko vitatu vinavyofanya kazi ya kuvusha abiria, mizigo na magari ambavyo ni MV Sengerema, Mv Mwanza na Mv Misungwi.
Wakizungumza na Nukta habari leo Januari 18 baadhi ya abiria waliofika kivukoni hapo wamesema wamekuta kivuko kimoja tu kukifanya kazi.
“Hatujui tatizo ni nini tumefika hapa toka saa 9 alasiri (Januari 17, 2022) tukakuta foleni ndefu hadi saivi saa 4 usiku bado hatujavuka, ” amesema mmoja wa wasafiri aliyejitambulisha kwa jina la Aloyce Kusekwa
Kusekwa ameiomba Serikali kama kuna tatizo kivukoni ni vema matangazo yawe yanatolewa ili kuondoa usumbufu kwa kuwa wapo watu wanaharaka na wengine wanarudisha watoto shule.
Amesema changamoto hiyo imesababisha baadhi ya abiria kugeuza magari kwenda kuvuka upande mwingine wa Kamanga.
Soma zaidi:
- Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia
- Majaliwa aagiza ubora wa barabara kuu Tanzania uangaliwe upya
Akizungumza changamoto hiyo, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Temesa Mkoa wa Mwanza, Hassan Karonda amesema amezungumza na mkuu wa kivuko hicho na kueleza kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa mvua kubwa eneo hilo iliyoambatana na upepo mkali.
Amewatoa wasiwasi wasafiri kuwa hali ya usafiri itarejea kawaida mawimbi yakitulia.
” Hadi sasa eneo la Kigongo Busisi kuna mvua kubwa na mawimbi makali hali ikitulia usafiri utarejea kama kawaida, ” amesema Karonda.
Pamoja na sababu hizo huenda kukamilika kwa daraja linaloendelea kujengwa kwenye kivuko hicho kutaondoa changamoto ya wasafiri kutumia muda mrefu kusubiri kivuko kwenda upande wa pili.
Kwa sasa wasafiri wanalazimika kutumia takribani dakika 15 hadi 30 wakiwa wanasubiri kuvuka.
Ujenzi wa daraja la JPM ambao unagharimu zaidi ya Sh699 bilioni kwa sasa umefikia asilimia 34 na unatarajiwa kukamilika February 2024.
Latest