Majaliwa aagiza ubora wa barabara kuu Tanzania uangaliwe upya

March 11, 2020 6:11 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza kufanyika ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote yaliyopo kwenye barabara kuu ili kujiridhisha na usalama wake. 
  • Ashangaa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote yaliyopo kwenye barabara kuu ili kujiridhisha ubora na usalama wake. 

Waziri Mkuu alikuwa akizungumza jana (Machi 10, 2020) wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, mara baada ya kutembelea daraja la Kiyegeya lililobomoka wiki iliyopita na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha mawasiliano na mikoa mingine.

“Nilitoa agizo kwa mameneja wa TANROADS ambao wana highways (barabara kuu), wazikague kila mara kwa sababu hatuhitaji kuwa na highways zilizobomoka,” amesema Majaliwa.  

Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu alibaini kuwa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.

“Uamuzi niliochukua wa kumhamisha Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu Bwana anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine. Fedha ya ukaguzi ipo, ya ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki. Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo, ateuliwe Meneja mwingine. 

“Nilimuuliza meneja aliyekuwepo kama wana fedha za ukaguzi, akasema anayo. Nikamuuliza kama anayo fedha ya spot maintenance (marekebisho ya dharura), akasema anayo. Fedha hizi zote zilipaswa zitumike kwa kazi iliyopangwa, lakini hilo halikufanyika,” amehoji Majaliwa.


Soma zaidi: 


Akijibu hoja hiyo, Mtendaji mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale alisema amemuacha Mhandisi Andalwisye aendelee kuwepo pale site (kazini) kwa sababu ya utalaamu wake kweye madaraja.

“Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi, tunatumia tu utaalmu wake,” amesema Mhandisi mfugale

Alipoulizwa kama ameshateua Meneja mwingine wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua mtu mwingine. 

Jumatano iliyopita, (Machi 4, 2020) Waziri Mkuu alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako alishuhudia mlundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.Aliagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea kutimiza wajibu wake.

Enable Notifications OK No thanks