Polisi wawasaka ndugu wa wanawake watatu waliofariki kando ya mto
- Miili yao imekutwa na majeraha kando ya mto uliopo Mtaa wa Mecco Kusini mkoani Mwanza.
- Polisi yaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
- Yaanza kutoa matangazo kuwatafuta ndugu wa marehemu.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema wakati linaendelea na uchunguzi wa vifo vya wanawake watatu ambao miili yao imekutwa kando ya mto karibu na Kituo cha Afya Buzuruga jijini hapa, linawatafuta ndugu wa marehemu hao ili kukamilisha taratibu za mazishi.
Wanawake hao ambao miili yao haijatambulika na wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30 wamekutwa wameuawa kando ya mto uliopo nyuma ya kituo cha afya Buzuruga katika mtaa wa Mecco Kusini mkoani Mwanza.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza,Gidion Msuya amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Januari 19, 2022 na uchunguzi wa vifo hivyo unaendelea kwa sababu watu hao hawajafahamika majina na sehemu wanakoishi.
Hata hivyo, Kamanda Msuya amesema wameanza kutoa matangazo ya kuwatafuta ndugu wa wanawake hao baada ya kuona hakuna dalili za watu kwenda kuulizia watu hao katika vituo vya polisi.
“Uchunguzi wa mauaji ya wanawake hao bado unaendelea na mpaka sasa bado hatujapata taarifa za ndugu wa marehemu kama polisi hatua tuliyofikia ni kuanza kuwatafuta ndugu zao kwa kutoa matangazo kwenye vyombo mbalimbali vya habari,” amesema Msuya.
Soma zaidi:
Kwa mjibu wa Msuya, upo muda wa kisheria ambao unatengwa iwapo hakutakuwa na ndugu atakayejitokeza basi Serikali kupitia kitengo cha afya nitachukua jukumu la kuihifadhi miili hiyo.
“Kuna muda wa kisheria huwa unatengwa kulingana na unyeti wa tukio lenyewe ukishapita bila ndugu kuonekana hatua zingine hufuata katika kuwahifadhi,” amesema Msuya.
Salamu za pole
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesema imepokea kwa masikitiko mauaji ya wanawake hao na imetoa pole kwa ndugu na jamaa, marafiki na wafiwa wote walioguswa na msiba huo mzito.
“Wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, Wizara inaendelea kukemea vikali vitendo vyote vya ukatili ikiwemo tukio hilo la mauaji,” imeeleza taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa leo.
Latest