Polisi yatoa ufafanuzi zaidi askari anayedaiwa kujinyonga mahabusu Mtwara
- Ni askari Grayson Mahembe anayedaiwa kujinyonga mahabusu.
- Jeshi la Polisi lasisitiza kuwa alijinyonga.
- Marehemu na wenzake saba wanatuhumiwa kumuua mfanyabiashara wa madini.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa askari wake Grayson Mahembe aliyefariki mkoani Mtwara akiwa mahabusu akikabiliwa na tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis kuwa alijinyonga.
Inadaiwa Mahembe alijinyonga Januari 22 mwaka huu kwa kutumia tambala la kudekia akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mtwara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mtwara ACP Mark Njera, Mahembe na askari wenzake saba wanatuhumiwa kutekeleza mauaji ya Hamisi (25), mkazi wa kijiji cha Ruponda Wilaya ya Nachingwea mkoani humo na kisha kumpora Sh70 milioni.
Watuhumiwa hao saba waliofikishwa Mahakamani Januari 25, 2022 ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango na Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Kisinza.
Wengine ni Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Msuya Mganga, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.
Imeelezwa kuwa tukio la mauaji ya kijana huyo walilitekeleza Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu waliutupa katika kitongoji cha Majengo, Kijiji cha Hiari wilayani Mtwara.
Baada ya kifo cha Mahembe kumekuwa na mjadala mpana hasa katika mitandao ya kijamii kuhusu mazingira ya kifo chake huku wengine wakihoji inawezekanaje mtu akajinyonga kwa tambala la kudekia.
Soma Zaidi:
Kutokana na mjadala huo, Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi zaidi na kusisitiza kuwa askari huyo alijinyonga na siyo vinginevyo.
Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime akieleza mazingira ya kujiua kwa askari huyo leo Januari 31, 2022 amesema baada ya watuhumiwa kufanya mauaji hayo hawakutoa taarifa kwa viongozi wao kwa sababu walifahamu kuwa wamefanya hivyo kwa nia ovu, kwa tamaa zao na kinyume cha sheria za nchi.
“Baada ya taarifa za tukio hilo kuwafikia viongozi wa Polisi Mkoa wa Mtwara, walianza uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwakamata askari waliokuwa wanatuhumiwa,” amesema Misime.
Misime amesema baada ya hatua hiyo Mahembe aliwekwa katika mahabusu ya peke yake na ndivyo pia ilifanyika kwa wale askari wengine kwani hata baadhi yao ilibidi wapelekwe mahabusu za Mkoa wa Lindi ili wasiharibu ushahidi uliokuwa unaendelea kukusanywa.
Amefafanua zaidi kuwa baadaye ndipo ikagundulika Mahembe amejinyonga na taratibu zote za ukaguzi wa matukio zilifuatwa ikiwepo kupiga picha kwa kutumia wataalam wa kuchunguza matukio kama hayo.
“Picha hizo zinaonesha dalili zote za mtu aliyejinyonga. Mwili ulifanyiwa uchunguzi pia (postmoterm) na daktari wa kuweza kuthibitisha kama kifo kilitokana na kujinyonga au ni sababu zingine,” amesema Misime.
Mwili wa Mahembe ulizikwa Januari 25 mwaka huu mkoani Iringa, huku wazazi wake wakilitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kifo chake hicho chenye utata.
Ufafanuzi kuhusu mazishi yake
Licha ya askari huyo kujiua alizikwa kawaida tofauti na askari wengine mbapo utaratibu maalum hufuatwa.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Misime amesema askari yeyote anayefariki katika hali ya kujitoa uhai, hazikwi kijeshi, kwa maana kuwa hakuna gwaride la mazishi litakalochezwa na risasi au mabomu ya kishindo kupigwa, kwani anahesabiwa kama hajafa kishujaa na hastahili heshima hiyo.
“Taratibu nyingine hufanyika kama kumpeleka katika eneo atakalozikwa kulingana na matakwa ya familia na ndivyo ilivyofanyika,” amesisitiza Misime.
Latest