Instagram yaja na mpango wa kuwatajirisha watumiaji wake

January 25, 2022 7:56 am · Wilson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imetengeza mfumo kuwawezesha watengeza maudhui kujipatia kipato.
  • Watapata fedha baada ya wafuasi wao kuona maudhui yao.
  • Mpango huo ni katika kutambua na kukuza talanta za watumiaji.

Dar es Salaam. Mtandao wa Instagram unakusudia kuja na mpango mpya wa kuwanufaisha watengeneza maudhui kwa kuongeza kipengele kipya kitakachowawezesha watumiaji kujisajili (subscribe) ili kupata maudhui kutoka katika kurasa za watengeneza maudhui.

Instagram inayokadiriwa kuwa na  watumiaji zaidi ya bilioni 1 ulimwenguni kote, mwaka 2020 pekee ilitengeneza mapato ya Dola za Marekani bilioni 24 (Sh Trilioni 55.3) kwa mujibu wa tovuti ya business of apps.

Katika hatua za kuboresha huduma za watumiaji wa mtandao huo, Instagram imetambua mchango wa watengeneza maudhui jinsi wanavyogusa na kubadili maisha ya watu kupitia talanta na ubunifu wao hivyo kuanzisha utaratibu wa kuwawezesha kupata malipo kutoka kwa wafuasi wao.

“Watayarishaji  huhamasisha watu ulimwenguni  kote kwa talanta zao na kusukuma utamaduni mbele kila siku. Katika Meta, tunaamini kwa dhati kuwezesha watayarishaji kupata riziki kupitia mifumo yetu na tumeunda safu ya zana za kuwaruhusu kufanya hivyo, kuwasaidia kupata usaidizi kutoka kwa watazamaji wao, kushirikiana na chapa na kupata pesa kutokana na utangazaji au bonasi moja kwa moja kutoka  Instagram,” imesema timu ya mauzo ya Instagram.

Tayari Instagram uliyoanzishwa mwaka 2010  imeanza majaribio ya kuwezesha mfumo huo mpya ambao utawahitaji watumiaji kujisajili (subscribe ) katika akaunti za watengeneza maudhui ili kupata idhini ya kutazama maudhui hayo ambapo yatakuwa na sifa zifuatazo;

  • Mubashara, mtandao huo utawaruhusu watengeneza maudhui kwenda mubashara moja kwa moja  kwa wafuasi wao waliosajiliwa.
  • Beji ya uanachama, (Subscriber’s badge). Watengeneza maudhui wataona beji katika ujumbe na maoni ya wafuasi wao ili kuweza kutambua kwa urahisi waliojisajili.
  • Hadithi za Wafuatiliaji. Watayarishaji wanaweza kuunda hadithi kwa ajili ya waliojisajili pekee, na kuwaruhusu kushiriki maudhui ya kipekee na kutumia vibandiko vya hadithi shirikishi na wafuasi wao waliojisajili tu.

Majaribio ya mfumo huo yamefanyika kwa  baadhi ya watengeneza maudhui  na tayari yameanza huko nchini Marekani kabla ya kurasimishwa ulimwenguni kote.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW