Afariki dunia akijenga daraja la Magufuli

February 14, 2022 3:36 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Ujenzi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ukiendelea. Picha| Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


  • Ni muongoza mitambo, Twalib Abbas aliyezama Ziwa Victoria.
  • Amefariki dunia wakati akijenga daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza.
  • Serikali yato maagizo usalama wa wafanya kazi katika mradi huo.

Mwanza. Mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Twalib Abbas amefariki dunia baada ya mtambo wa kunyanyau vitu vizito aliokuwa akiuongoza kutumbukia katika Ziwa Victoria wakati ujenzi wa daraja la Magufuli mkoani Mwanza ukiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel aliyekuwa akizungumza eneo la tukio jana Februari 13, 2022 amesema mwili wa marehemu tayari mwili umeopolewa kutoka majini na kuhifadhiwa huku uchuguzi wa tukio hilo ukiendelea.

“Tulipokea taarifa za ajali hii majira ya saa 8 au tisa usiku (Usiku wa kuamkia Februari 13)  ambapo operator (muungozaji) alikuwa ameingia shifti ya usiku ndipo ajali ilipotokea,” amesema Mhandisi Gabriel. 

Mtambo uliozama ndani ya Ziwa Victoria ni kijiko chenye uzito wa Tani 55 na chanzo cha ajali bado kinachunguzwa. 

“Chanzo cha ajali kinachunguzwa na kimetokea wakati operator akiwa kwenye daraja la muda lenye upana wa mita 9 lakini alishindwa na kuanguka kwenye kina kirefu cha maji, ” amesema.

Kwa sasa wanaangalia namna gani wataweza kutoa hicho kifaa ingawa uongozi umebainisha kuwa na kifaa chenye uzito wa tani 80 ambacho kitatumika katika uokoaji. 

Aidha, Gabriel ameutaka uongozi wa kampuni inayojenga daraja hilo kuzingatia sheria ya usalama mahali pa kazi ili kuwalinda wafanya kazi wasipate madhara yanayoweza kuzuilika.

Daraja hilo la Kigongo-Busisi litakapokamilika litarahisisha shughuli za usafiri kwa wakazi wa Mwanza na Mkoa wa Geita na nchi jirani za maziwa makuu na hivyo kupunguza uhitaji wa vivuko katika eneo hilo.

Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2  na kugharimu zaidi ya Sh716 bilioni kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 30. 

Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Mwanza, Ambwene Mwakibete amesema baada ya kupokea tarifa za tukio hilo, usiku walishindwa kumuokoa marehemu na badala yake zoezi lilifanikiwa kufanyika asubuhi. 

Ameutaka uongozi unaojenga daraja hilo kuhakikisha linafata maelekezo  yanayotolewa pamoja  na kuzingatia utaalamu wa kazi zao. 


Soma zaidi: 


Mmoja wa dugu wa marehemu, Mohamed Yassin  amesema kinachofuata hivi sasa ni familia  kukaa pamoja na kupanga taratibu za mazishi. 

Amesema marehemu alikuwa mzoefu wa kazi hizo na amewahi kufanya kazi kwenye madaraja mbalimbali nchini. 

Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litatatua kero ya miaka mingi iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.

Daraja hilo lililopewa jina la Hayati Rais Magufuli, ujenzi wake utakamilika mwaka 2023.

Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo, Abdlkareem Majuto amesema ajali ya mfanyakazi kuanguka au kuzama ziwani si ya kwanza kutokea tangu waanze ujenzi wa daraja hilo.

Amesema mpaka sasa wameshuhudia ajali tatu za watu kuzama ziwani na kinachofanyika kwa wahanga ni kulipwa stahiki zao zote ikiwemo gharama za kusafirisha mwili.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW