Daraja la Magufuli kuachilia neema vivuko Ziwa Victoria
- Likikamilika hakutakua na haja ya kutumia vivuko.
- Vivuko vilivyopo katika eneo hilo kupelekwa maeneo mengine.
- Daraja hilo litakamilika mwaka 2023.
Mwanza. Serikali imeiagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kuanza mchakato wa kutathmini maeneo yenye uhitaji ambayo yatapelekewa vivuko vinavyofanya kazi katika eneo la Kigongo- Busisi mara tu ujenzi wa daraja la Magufuli litakapokalika.
Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 ambalo lingharimu zaidi ya Sh716 bilioni kwa sasa umefikia asilimia 30.
Kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha shughuli za usafiri kwa wawakazi wa Mwanza na Mkoa wa Geita na nchi jirani za maziwa makuu na hivyo kupunguza uhitaji wa vivuko katika eneo hilo.
Naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza leo Novemba 15, 2021 baada ya kukagua vivuko vinavyofanya kazi ndani ya Ziwa Victoria, amesema baada ya miaka miwili daraja hilo litakamilika hivyo ni vyema Temesa ikaanza kufanya maandalizi ya kuvihamisha vivuko hivyo.
“Hapa kuna vivuko kimoja kina beba tani 250 na kipo kingine kina beba tani 170 na Ziwa Victoria lina uhitaji mkubwa wa vivuko, mnaweza msivipeleke vyote sehemu moja lakini mnaweza kuangalia wapi ambapo kuna uhitaji mkubwa wa vivuko mkavipeleka huko,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Waziri huyo amesema daraja litakapokamilika vivuko vitakuwa havina kazi, wafanye utafiti waone ni sehemu gani vitaenda kufanya kazi kwa mapato sawa sawa na hapo vinapotoka.
”Tukiangalia Ziwa letu lina visiwa vingi vingine vipo Ukerewe vingine Bukoba hivyo waangalie ni wapi vivuko hivyo vitaenda kufanya kazi na kukusanya mapato,” amesisitiza naibu waziri huyo.
Amesema katika kivuko cha Kigongo-Busisi kuna vivuko vitatu ambavyo ni Mv Mwanza, Mv Sengerema na Mvi Misungwi na vivuko hivyo ni vya pili kwa ukusanyaji wa mapato kikitanguliwa na kile cha magogoni Dar es Salaam.
Moja ya kivuko kinachofanya safari zake kati ya Mwanza na Geita cha Mv Sengerema. Picha| Mariam John.
Waziri Kasekenya pia ameagiza kufanyiwa maboresho ya miundombinu ya majengo ambayo abiria walikuwa wanakaa kusubiria kuvuka kugeuzwa kitega uchumi kingine.
“Temesa wafikiri baada ya daraja kuanza kazi haya majengo yatafanya nini? kuna miundombinu mikubwa wanaweza kuanzisha karakana, chelezo au maeneo ya biashara kwa siku za baadaye hivyo ni vyema masuala haya wayaangalie ni kwa namna gani miundombinu hiyo itafanya kazi,” amesema.
Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litatatua kero ya miaka mingi iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.
Daraja hilo lililopewa jina la Hayati Rais Magufuli, ujenzi wake utakamilika mwaka 2023.
Soma zaidi:
- Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia
- Majaliwa aagiza ubora wa barabara kuu Tanzania uangaliwe upya
- Daraja la Kigongo Busisi litakavyoinua uchumi kanda ya ziwa
Mtendaji Mkuu wa Temesa, Temesa Hasan Kalonda, amesema maelekezo ya naibu waziri huyo wameyapokea na watayafanyia kazi na kwamba katika Mkoa wa Mwanza hakuna sehemu ya karakana hivyo wanaweza kufikiria kuanzia hapo.
Kuhusu utolewaji wa huduma kwenye vituo hivyo unaendelea vizuri na kuna baadhi ya vivuko kama Kigongo- Busisi wanatoa kwa masaa 24 ispokuwa kisiwa cha Kisorya ambapo wanatoa kwa masaa 12.
Latest
