Neema inakaribia, ujenzi daraja la Magufuli ukishika kasi
Wajumbe wa Bodi ya Barabara wakipata maelezo ya ujenzi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi mkoani Mwanza wakati walipotembelea jana Julai 20, 2022 ili kujiridhisha ujenzi unavyoendelea. Picha | Mariam John.
- Ujenzi wa daraja la JPM Kigongo_Busisi mkoani Mwanza umefikia asilimia 48.9.
- Litakamilika mwaka 2024 na kugharimu zaidi ya Sh600 bilioni.
- Litaondoa changamoto usafiri wa majini Kanda ya Ziwa.
Mwanza. Ujenzi wa daraja la JPM Kigongo_Busisi mkoani Mwanza umefikia asilimia 48.9, jambo linalotia matumaini kwa wananchi wanaotumia Ziwa Victoria kuondokana na tatizo la ukosefu wa usafiri wa uhakika wa majini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Joseph Haule ambaye aliongozana na wajumbe wa bodi hiyo katika ziara maalum ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo jana Julai 20, 2022 amesema kutokana na maelezo yaliyotolewa na wasimamizi wa mradi imetoa matumaini ya daraja hilo kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Haule amesema licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zilizojitokeza lakini mkandarasi anayetekeleza mradi ameonyesha jitihada katika kazi hiyo.
“Wametueleza changamoto ya kina cha maji kuongezeka tofauti na matarajio yao. Pia uwepo wa miamba mingi ndani ya ziwa na ugonjwa wa Uviko-19 kukwamisha baadhi ya malighafi kufika nchini lakini kwa kweli wanaendelea vizuri na ujenzi na sisi kama Bodi ya Mfuko wa Barabara tumeridhika,” amesema Haule.
Ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 48.9 na mkandarasi yuko kazini kuhakikisha kazi hiyo inakamikika kwa wakati uliopangwa.
Daraja hilo ambalo limepewa jina la John Magufuli linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita na nchi za maziwa makuu likikamilika litakuwa na urefu wa kilomita 2.3 na upana mita 28.45 na ujenzi wake utagharimu Sh699 bilioni.
Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza vinavyofanya safari zake Ziwa Victoria.
Licha ya daraja hilo ambalo litakamilika 2024 kutatua tatizo la usafiri wa majini, pia litaufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kivutio kikuu cha utalii na biashara kwa nchi za maziwa makuu.
Mhandisi mshauri wa ujenzi wa daraja hilo, Abdulkareem Majuto amesema tayari nguzo 22 zimeinuliwa katika zoezi la ulazaji wa nguzo linaloendelea katika ujenzi huo.
“Kwa sasa mkandarasi anaendelea na zoezi la kuinua nguzo katika daraja hili na mpaka sasa tayari wameshainua nguzo 22 na bado kazi inaendelea,” amesema Mhandisi Majuto.
Latest