TMA inavyojiimarisha utoaji taarifa sahihi za hali ya hewa
- Inakabiliana na vikwazo mabadiliko ya hewa.
- Imeongeza miundombinu ikiwemo vituo vya hali ya hewa.
- Inashirikiana na sekta binafsi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema licha ya kupiga hatua kubwa katika utabiri wa hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ili kutoa taarifa sahihi za hali hewa zenye mchango mkubwa katika maendeleo
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha mamlaka hiyo, Samuel Mbuya amesema mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto ni changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiingilia utendaji wa mifumo ya hali ya hewa na hivyo kutatiza uchakataji wa taarifa za hali ya hewa.
Amesema changamoto hiyo hutokea zaidi katika upatikanaji wa taarifaza hali ya hewa hasa katika maeneo madogo ambayo yameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
“Endapo kutatokea uharibifu wa mazingira au mabadiliko ya tabianchi, ina maana kuwa mifumo yetu inachukulia kuna msitu hapa na ule msitu unatoa uchafu fulani na inaingiza kwenye mifumo ya hali ya hewa. Sasa kama huo msitu haupo utakuwa umeingiza taarifa ambazo siyo sahihi,
“Lakini kitu kingine kinachoweza kutokea ni kwamba unapokuwa na ongezeko la joto duniani, nayo pia inaweza ikasababisha mifumo yetu ya utabiri ikawa ikapata changamoto,” amesema Mbuya wakati akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Amesema changamoto wanazokabiliana nazo ni za kisayansi zaidi, hivyo hutumia njia mbalimbali kukabiliana nazo ili kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na sekta mbalimballi.
“Hatua ambazo zinachukuliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa moja ni kuongeza mtandao wa vituo ili uweze kupata taarifa za kina zaidi za maeneo madogo madogo ili hayo mabadiliko yanayotokea sasa uweze kuyapima na kuyaingiza kwenye mifumo ya kuchakata taarifa,” amesema Mbuya.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini.
Mbuya aliyekuwa akizungumza katika warsha ya waandishi wa habari kuhusu utabiri wa mvua za masika Februari 15, 2022 amesema Serikali imekuwa ikitenga bajeti kuongeza miundombinu ya ufuatiliaji ikiwemo ununuzi wa rada, vituo vinavyojiendesha vyenyewe katika maeneo mbalimbali.
“Ni wazi kwamba nchi yetu ni kubwa na hali hewa inabadilika kwa kiwango kikubwa kutoka eneo moja na jingine,” amesema mtaalam huyo wa masuala na hewa.
Serikali kupitia sheria namba 2 ya 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa majukumu kwa mamlaka hiyo kuratibu na kudhibiti shughuli za hali ya hewa Tanzania ili kutoa fursa kwa wadau ikiwemo sekta binafsi kutoa mchango wao hasa kuboresha vituo vya hali ya hewa.
Amesema licha kushirikiana na sekta binafsi wanadhibiti ubora wa takwimu zinazopatikana ili zichakatwe vizuri kuleta matokeo sahihi yanayoendana na hali ya hali ya hewa ya eneo husika.
Taarifa sahihi za hali ya hewa huwawezesha wananchi na sekta mbalimbali kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kuchukua stahiki dhidi ya hali mbaya ya hewa katika maeneo yao.