Mambo ya kufanya kujikinga na uvamizi wa wanyamapori wakali
- Kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa uhifadhi.
- Kujiepusha na tabia ya kupambana na wanyamapori wanapoingia kwenye maeneo yao.
Dar es Salaam. Ikiwa unaishi karibu na mbuga za wanyama na umekuwa ukiingia katika migogoro na wanyamapori mara kwa mara, usihofu kwa sababu unaweza kuchukua hatua muhimu kujikinga na madhara ya wanyama hao.
Migogoro ya binadamu na wanyamapori wakiwemo tembo imekuwa ikisababisha madhara mbalimbali ikiwemo uhalibifu wa mali na makazi, majeraha, ulemavu na hata vifo vya watu.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara za kiuchumi na kuwatumbukiza baadhi ya watu katika umaskini pale miradi yao inapoharibiwa na wanyamapori wanaovamia katika makazi yao ambayo wakati mwingine huwa ni mapitio ya wanyama (shoroba).
Shoroba hutumika na wanyama kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutafuta chakula na maji na kutafuta makazi ya muda.
Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa mwongozo unaotoa maelekezo ya namna ya kujikinga na uvamizi wa wanyama wakali kwa watu wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na maeneo tengefu.
Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana katika mwongozo huo uliotolewa Mei 2022 amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kudhibiti wanyamapori, wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wanatakiwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa uhifadhi ili kuepuka madhara yatakayosababishwa na wanyamapori hao.
“Wananchi wajiepusha kuwasogelea wanyamapori, kuchukua tahadhari kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo au pembezoni mwa hifadhi, maeneo yenye mamba na viboko, mapito na mtawanyiko wa wanyamapori,” amesema Dk Chana.
Wametakiwa kujiepusha na tabia ya kupambana na wanyamapori wanapoingia kwenye maeneo yao, kutoshiriki katika zoezi la kufukuza wanyamapori wakali na waharibifu kwa wazee, watoto, wajawazito, wenye changamoto mbalimbali za ulemavu, na waliotumia kilevi.
Matembezi yasiyo ya lazima nyakati za usiku kwa wananchi waishio pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa hayashauriwi na ikibidi basi watembee zaidi ya mtu mmoja.
Wavuvi watahadharishwa
Dk Chana anasisitiza wavuvi kuepuka uvuvi hatarishi hususani kuvua nyakati za usiku katika maeneo yenye mito na maziwa yaliyopo karibu na hifadhi.
“Epukeni matumizi ya vifaa duni pamoja na kutoa taarifa za matukio ya uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu haraka kupitia namba za kupiga simu bure zilizotangazwa na wizara,” amesema waziri huyo ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais.
Wanyamapori hatarishi
Wizara hiyo imefanya tathmini na kubaini kuwa wanyamapori hatarishi na waharibifu ni pamoja na tembo, simba, mamba na viboko ambao matukio yao yamekuwa yakijirudia hasa katika wilaya 53 kati ya 134 nchini.
Aidha, Serikali imeahidi kushirikiana na wananchi kuwadhibiti wanyamapori hatarishi na itaendelea kutoa kifuta jasho na machozi kwa mujibu wa taratibu za kisheria kwa wananchi wote walioathirika na watakaoathirika.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Sababu za migogoro ya binadamu na wanyamapori
Migongano hii husababishwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame wa muda mrefu na mafuriko na kupungua kwa malisho kunakosababishwa kuenea kwa mimea vamizi katika baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Uchungaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa husababisha wanyamapori kutoka kwenye maeneo ya hifadhi na hivyo kuongeza migongano kwenye maeneo ya wananchi.
Matumizi holela ya ardhi na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu hasa katika maeneo ya jirani na hifadhi yakiwemo shoroba na mtawanyiko wa wanyamapori.
TANGAZO: Daima tuko na wewe katika kukupatia habari zinazokuhusu. Wenzako wamejiunga na jumuiya yetu ya Telegram ya @NuktaHabari, wewe unasubiri nini? Unaweza kujiunga kupitia kiunganishi hiki>> https://bit.ly/2TeLWIn