Serikali yatangaza kiama kwa wanyama wanaozurula mitaani
- Ni pamoja na mbwa wanaozurula mitaani wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
- Hatua hiyo itasaidia kuepusha hatari ya maambukizi ya magonjwa kwa binadamu.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewaagiza maafisa ugani nchi nzima kudhibiti ongezeko la mifugo inayozurula hovyo mitaani ikiwemo mbwa ili kuzuia hatari za magonjwa kama kichaa cha mbwa (rabies) kwa wakazi wa maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum wa mkoa wa Kilimanjaro, Esther Maleko, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kudhibiti hali hiyo.
“Mbwa akizurura mtaani kwako na hana mwenyewe na Serikali za mitaa zikajiridhisha kwamba hana pa kwenda na pengine ameshapata maambukizi ya kichaa cha mbwa, hatua stahiki ambazo tumeisha waelekeza ni pamoja na kuwaondoa duniani ili wasilete madhara kwa binadamu,” amesema Mnyeti.
Kwa mujibu wa takwimu za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Tanzania ina mbwa milioni 4.5 huku asilimia 98 ya mbwa hao wakiwa hawaana usimamizi na huishia kuzurura mitaani.
Takwimu hizo zinabainisha kuwa mbwa hao ni wengi zaidi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Iringa, Tabora na mikoa yote ya kanda ya ziwa ambapo wafugaji wengi wanaishi.
Aidha, Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa kichaa cha mbwa husababisha takriban vifo 70,000 dunaini kote kila mwaka huku nchini Tanzania watu 15,339 wakiripotiwa kupata ugonjwa huo mwaka 2022
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe alisema idadi hiyo iliyorekodiwa katika kipindi cha miezi nane hadi Agosti 2022 imepungua kutoka matukio 39,787 yaliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2021.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na uvuvi, Alexander Mnyeti akijibu maswali bungeni, jijini Dodoma.
Aidha, Chapisho la tovuti ya Gazeti la Mwananchi la Septemba 29, 2022 lilimnukuu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Hezron Nonga akisema kuwa kwa wastani watu 3,387 hung’atwa na mbwa kila mwaka, hivyo kuwa kwenye hatari ya kuambukizwa kichaa cha mbwa kinachoenezwa pia na mbwa mwitu, paka, fisi na popo.
kutokana na madhara yanayotakana na wanyama hao kuzagaa, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Sura ya 154 inatoa mwongozo kuhusu haki za wanyama na ikisitiza wafugaji kutunza mifugo yao.
Kupitia Sheria hiyo kila mfugaji anawajibika kuhakikisha kuwa mifugo yake inapata matunzo bora, ikiwa ni pamoja na chakula na mazingira safi.
Mfugaji atakayeshindwa kutunza vyema anaweza kutozwa faini ya Sh50,000 hadi Sh300,000 au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote mbili kama ilivyoanishwa na Sheria ya Serikali za Mitaa ya Mjini na Vijijini ya mwaka 1982.
Ili kuepusha maradhi kwa wanyama wanaofugwa majumbani, mfugaji anapaswa kuhakikisha mifugo yake imechanjwa, hiyo itamsaidia kuepukana na faini au kifungo pamoja na kulinda afya za watu wengine.