CCM yaadhimisha miaka 48, ikijipanga kwa ushindi uchaguzi mkuu 2025

February 5, 2025 7:03 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Yajipanga kuzitumia jumuiya za chama ikiwemo ya wazazi kueneza mema yaliyofanywa  na chama hicho.
  • Vijana wa chama hicho kunolewa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezitaka jumuiya za chama hicho kuweka mikakati thabiti ya ushindi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma, leo Februari 5, 2025, Rais Samia amezitaka jumuiya hizo ikiwemo wanawake, wazazi na vijana kutumia mbinu za kisasa kushinda uchaguzi huo.

“Nataka niwape mfano wa jinsi tulivyofanya vizuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kama mwenyekiti, niliwatumia wanachama wangu wote ujumbe wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura,” amesema Rais Samia.

CCM inasherekea miaka 48 tangu kuanzishwa kwake ikijivunia kusalia madarakani kwa miaka 33 mfululizo, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

CCM inasherekea miaka 48 tangu kuanzishwa kwake ikijivunia kusalia madarakani kwa miaka 33 mfululizo, Picha | Global Publishers

Katika miaka hiyo, viongozi wa awamu sita kutoka chama hicho wameiongoza Tanzania tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kufanya maadhimisho hayo huku kikiwa kinajiandaa na uchaguzi mkuu ambao tayari vugu vugu lake limeshaanza baada ya chama hicho na baadhi ya vyama pinzani kutangaza wagombea katika nafasi ya urais.

Ili kujihakikishia ushindi Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi alisema kuwa chama hicho kinaitegemea Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ambao takwimu zinawataja kuwa wengi zaidi kuliko jumuiya nyingine ndani ya chama hicho.

“Tunajua kwamba kushinda tutashinda lakini tunataka ushindi wa kishindo…na jeshi tunalolitegemea kuliko majeshi yetu yote ni jeshi la wanawake (UWT).” amesema Dk Nchimbi alipokuwa akizungumza katika kongamano la jumuiya hiyo Februari 4, mwaka huu,

Mbali na Jumuiya hiyo Rais Samia ameutaja Umoja wa Vijana kama silaha ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu na chaguzi nyingine zijazo ambapo wanatakiwa kupikwa na kuandaliwa vyema kushika hatamu ya chama hicho.

“Ni lazima tuwekeze kwa vijana na kuwajenga kiitikadi ili waelewe vizuri siasa ya nchi yetu na misingi ya kuanzishwa chama chetu… 

…Kesho salama ya chama chetu na nchi yetu itahakikishwa kwa vijana wetu kujengewa uwezo ndani na nje ya nchi ili  waweze kujipanga kitaasisi na waweze kupambana kwa hoja na yeyote mwenye hoja hasi kwetu” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameutaja Umoja wa Vijana kama silaha ya kushinda uchaguzi mkuu Picha | Chama Cha Mapinduzi.

Kwa mikakati hiyo huenda CCM ikaendelea kuvutia zaidi kundi la Vijana ambalo Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inawataja kuwa 699,845.

Katika hatua nyingine Rais Samia amezitaka jumuiya hizo kuongeza juhudi za kuwatembelea wananchi na kuwaeleza mafanikio ya Serikali inayoongozwa na CCM ikiwa ni miongoni mwa mbinu za ushindi katika uchaguzi ujao.

“Ni dhahiri kuwa kila mwana-CCM ana jambo la kusema kuhusu maendeleo katika kijiji au kata yake. Hakuna eneo tuliloacha, kila mmoja ana ushuhuda wa mafanikio ya serikali yetu,” amesema Rais Samia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks