Wakulima waukwaa, bei ya mahindi ikipanda Tanzania

September 19, 2022 12:59 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Julai 2022 ilikuwa Sh87,383 ikipanda kutoka Sh43,371 mwaka jana.
  • Sababu ni kuongezeka kwa mahitaji na kupungua kwa mavuno.
  • Bei za mazao mengine ya chakula nazo zapanda.

Dar es Salaam. Wakulima na wafanyabiashara huenda ni miongoni mwa watu walionufaika zaidi na zao la mahindi baada ya bei ya jumla ya zao hilo kupanda zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya Agosti 2022 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Julai 2022 ilikuwa Sh87,383 ikipanda kutoka Sh43,371 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Hiyo ni sawa na kusema wakulima na wafanyabiashara wameweka kibindoni Sh44,012 zaidi kwa kila gunia moja au sawa na kusema bei hiyo ya mahindi imeongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na bei ya mwaka jana. 

Kupanda kwa bei kunawaumiza walaji kwa sababu wanalazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kupata zao hilo la chakula.

BOT katika ripoti hiyo imeeleza kuwa kupanda kwa bei ya mahindi kumechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo hasa nje ya nchi na kutokuwepo kwa mvua za kutosha katika msimu huu, jambo lililosababisha wakulima wapate mazao kidogo.

“Kuongezeka kwa bei kumechangiwa na mahitaji makubwa ya nchi jirani na kushuka kwa mavuno kutokana na mvua chache,” imeeleza BoT katika ripoti hiyo ambayo inapatikana katika tovuti yake. 

Pia miezi minne iliyopita, bei ya mahindi imekuwa ikipanda mfululizo. 

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.

Pia katika kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita bei za mazao mengine ya chakula zimepanda ikiwemo viazi mviringo na mchele.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW