Uchafuzi Mto Mirongo wawaweka hatarini watumiaji Ziwa Victoria

September 26, 2022 12:06 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mto huo uliopo Mwanza wakithiri kwa taka.
  • Wananchi hatarini kupata magonjwa ya mlipuko
  • Serikali yaingilia kati, yataka kila mtu awajibike kuutunza mto huo. 

Mwanza. Mto Mirongo ni moja vyanzo muhimu vya maji vya Ziwa Victoria.

Licha ya umuhimu wa mto huo uliopo mkoani Mwanza, uko katika hatari kukauka na kusababisha madhara ya kiafya na kimazingira kwa watu wanaoutumia kwa shughuli mbalimbali.

Hali hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa shughuli za binadamu ikiwemo kulima pembezoni mwa mto huo na utupaji wa taka.

Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  imeshuhudia taka ngumu ikiwemo chupa za plastiki zikiwa zimetuama kando ya kingo za mto huo ambazo kama mvua ikinyesha zitasukumwa na maji kuingia ziwani. 

Faustine Balele (54) amekuwa akiishi mtaa wa Mabatini jirani na mto huo anasema watu wanaozunguka mto huo hutupa uchafu wa aina mbalimbali ndani ya mto huo hali inayosababisha uchafu kujikusanya na kuziba kwenye kingo za mto.

“Hatari zaidi ni kwenye kipindi cha mvua ambapo mto unapofurika huzoa taka hizo na kwenda kuzimwaga ziwani,” anasema  Balele na kubainisha kuwa wakati mwingine uchafu huo huingia kwenye makazi na kuhatarisha afya za watu.

Mkazi mwingine wa jijini hapa, Amina Omary anasema tabia za uchafuzi wa mto huo hufanywa na wananchi wanaoishi kando ya mirongo pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo ambao hutupa taka taka zao ndani yam to huo.

Mto Mirongo unakabiliwa na hatari kubwa ya kukauka baada ya kukithiri kwa uchafu wa mazingira. Picha | Mariam John. 

Ni zaidi ya uchafuzi wa mazingira

“Utakuta taka hizo zote zinaingia ziwani wakati huo wapo wanaotumia maji hayo kunywa, kupikia na kuongea hivyo tunaiomba Serikali kuweka mikakati ya kudhibiti utupwaji wa taka hizo kwenye Mto Mirongo,” anasema Diana Kimario mkazi wa mtaa wa Uhuru jijini Mwanza.

Wakazi hao wamesema kitendo cha mto huo kuendelea kuchafuliwa kunaweza kusababisha magonjwa yakiwemo ya mlipuko.

Afisa Misitu na Mratibu wa shughuli za Mazingira Mkoa wa Mwanza, Mangabe Mnilago anasema wakazi wa mtaa wanaoishi kando na mto hutiririsha maji machafu yaliyochanganyikana na vinyesi hali inayosababisha kuwepo kwa magugu maji mengi ndani ya Ziwa Victoria.

Anasema ili mto huo uwe safi ni vyema wananchi wanaoishi kando na mtu huo waache tabia ya uchafu wa kutupa taka ovyo.

“Ni kweli kwamba mto huo unachafuliwa na watu wanaoishi kando na mto huo pamoja na wafanyabiashara, kinachofanyika hadi sasa Serikali inajitahidi kusafisha ili kudhibiti uchafu huo usiingie ziwani na kuzalisha magugu maji,” anasema Mnilago.


Soma zaidi:


‘Suluhu yapatikana’ 

Halmashauri ya Jiji la Mwanza imekuja na mikakati mbalimbali ya kudhibiti uchafuzi wa mto huo ikiwemo mfumo wa wakala wa ukusanyaji wa taka mitaani na kuzipeleka eneo maalum la kutupia taka.

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Yahaya Sekiete anasema mpaka sasa halmashauri hiyo ina magari 13 ya kukusanyia taka kutoka kwenye vituo 25 vya kutupia taka kisha hupelekwa kwenye dampo la taka lililopo Buhongwa.

Pia sheria mbalimbali zimewekwa ili kulinda uchafuzi wa mazingira ikiwemo faini ya Sh30,000 kwa mtu anayechafua mazingira lakini pia Sh5,000 kwa mwezi kwa kila kaya kwa ajili ya uchafu.

“Halmashauri pia inaendelea kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa kutunza mazingira ikiwemo kuacha tabia ya kutupa taka ovyo,” anasema Sekiete.

Kutokana na kupita karibu na makazi ya watu. Mtoto huo umekuwa ukichafuliwa na taka zinazotupwa na watu. Picha | Mariam John.

Hatua zingine zinazochukuliwa

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza hivi karibuni, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo  alisema zaidi ya tani 43.38 za mifuko ya plastiki imekamatwa na kuteketezwa toka sheria ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki na vifugashio vya mifuko hiyo kudhibitiwa.

Waziri Jafo alitaja moja ya madhara yanayoweza kujitokeza kwenye mifuko na taka za plasitiki kuwa ni kuharibu vyanzo vya maji na hivyo kusababisha matatizo kwa watumiaji.

Alisema Tanzania imejiwekea sheria na kanuni ambazo zinapiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ikiwa ni njia ya kulinda mazingira.

Waziri Jafo aliwahimiza wananchi na mamlaka za serikali za mitaa kuifanya nchi kuwa safi na kusisitiza suala la uwekaji vitunza takataka kwenye mitaa.

“Tuifanye nchi yetu iwe safi kabisa, niwaombe katika mamlaka za serikali za mitaa twende na suala la kuweka utamaduni wa kuweka dustbin (vihifadhia taka) kataka mitaa yetu,” alisema Jafo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW