Wafahamu washindi tuzo za ubora za Afrika Mashariki kutoka Tanzania
- Ni pamoja na kampuni ya Faima Products, Caps Limited na Bakhresa.
- Washinda katika vipengele vya vinara wa ubora kwenye uzalishaji na huduma.
- Tuzo hizo ni chachu ya kuzalisha bidhaa na huduma zenye ubora kupenya katika soko la kimataifa.
Dar es Salaam. Tanzania imefanikiwa kutoa washindi watatu katika tuzo za ubora za Afrika Mashariki za mwaka 2022 ili kuhamasisha wajasiriamali na wafanyabiashara kutengeneza bidhaa na huduma bora kuwawezesha kufaidika na soko la kimataifa.
Tuzo hizo (EAC Awards) zilizoshirikisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi zimegawanyika katika makundi mawili makuu ya vinara katika ubora kwenye sehemu ya uzalishaji na vinara katika ubora kwenye huduma.
“Kwenye sehemu ya uzalishaji kuna mshindi wa kwanza na wa pili. Na hapo kuna wajasiriamali wakubwa na wadogo,” amesema Mratibu wa tuzo hizo, Safari Fungo Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam.
Washindi kutoka Tanzania waliong’ara katika tuzo hizo ni kampuni ya Faima Product ambayo imeshika nafasi ya kwanza katika kipengele cha kinara wa ubora katika uzalishaji kwa kampuni ndogo na za kati.
Kampuni hiyo inayojihusisha na utengenezaji wa mafuta ya nywele, ngozi na kuoka vitafunwa yanayotokana na zao la nazi ilikuwa inashindanishwa na kampuni za Valle du Sacre Coeur na Sovert za Burundi na Kinazi Cassava Plant, Ltd ya Rwanda.
Caps Limited imeshinda kipengele cha kinara wa ubora kwenye huduma kwa kampuni ndogo na za kati.
Kampuni hiyo iliyoanzishwa 1997 imebobea katika kutoa huduma za ufukizaji, mifumo ya vyoo isiyo na maji ya kibayolojia, feni za ukungu, kukodisha mahema, utunzaji wa maji taka, vyoo vinavyohamishika kwa matukio ya nje/sherehe na bidhaa za usafi.
Caps Limited imeibuka mshindi baada ya kuipiku kampuni ya Water Access Rwanda ya nchini Rwanda.
Washindi wa tuzo za ubora za Afrika Mashariki kwa mwaka 2022 waliotangazwa leo jijini Dar es Salaam. Washindi hao wanatoka Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda. Picha| EACMarkup.
Washindi zaidi
Katika kipengele cha kinara wa ubora kwenye huduma kwa makampuni makubwa, mshindi wa kwanza aliyetangazwa ni kampuni ya Said Salim Bakhresa ambayo imekuwa ikijuhusisha na shughuli mbalimbali nchini ikiwemo huduma za usafiri, habari, vyakula na vinywaji.
Kampuni hiyo ambayo imeajiri watu wengi Tanzania ilikuwa inashinda na kampuni ya AC Group ya Rwanda ambayo imebobea katika kutoa huduma za suluhu za kidijitali za usafiri.
Lodhia Foods Products kutoka Burundi, ndiyo kampuni iliyoshinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha kinara wa ubora kwenye huduma kwa makampuni makubwa.
“Tuzo hizi ni sehemu mojawapo ya kuwatambua wajasiriamali na makampuni makubwa kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha kwamba bidhaa na huduma wanazozalisha zinakuwa zinakidhi mahitaji ya ubora na viwango katika nchi zao na vilevile katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Fungo.
Amesema pia zitawasaidia washindi kuwa katika nafasi nzuri ya kufaidika na masoko ndani ya jumuiya na kimataifa.
Katika tuzo hizo kulikuwa na washiriki 12 kutoka nchi tatu za EAC.
Mchakato wa kuwapata washindi hao ulianzia katika nchi zao kwa kuwapata washindi ambao walienda kushindanishwa na washindi wa mataifa mengine ya EAC.
Fungo amesema kigezo kikubwa kilichozingatiwa katika tuzo hizo ni uwezo wa kampuni kukidhi vigezo vya ubora kuanzia anavyopata malighafi, uchakataji na mpaka anapata bidhaa ya mwisho.
Pia anavyotoa huduma kwa wateja wake ikiwemo kuweka mifumo thabiti ya kushughulikia kero za wateja wake.