Wafanyabishara wanavyoweza kuongeza faida zao la kahawa Tanzania

March 29, 2022 1:21 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kupata maarifa ya kuandaa mikataba ya biashara.
  • Kufahamu kwa undani mnyororo wa thamani wa zao hilo.
  • Mwaka 2020, tani 64,000 za kahawa ziliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa Sh336.8 bilioni.

Dar es Salaam. Huenda upatikanaji wa soko kwa wafanyabiashara wadogo wanaojishughulisha na zao la kahawa nchini Tanzania ukaimarika zaidi, baada ya wadau wa zao hilo kuwaongezea ujuzi na maarifa wa namna ya kuendesha biashara hiyo.

Maarifa hayo yanalenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata ujuzi wa kusimamia mikataba ya kahawa, usafirishaji, uandaaji wa nyaraka, usindikaji na usambazaji.

Kwa muda mrefu wakulima wa kahawa Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na ujuzi hafifu wa namna ya kuandaa vyema mazao yao ili yaweza kupata soko zaidi la ndani na la kimataifa. 

Mtaalam wa kahawa kutoka Uganda, Robert Nsibirwa amesema ni muhimu wakulima na wafanyabiashara kuelewa vema masuala ya mikataba kwa kuwa biashara ya kahawa duiniani kote hufanyika kwa njia hiyo.

Nsibirwa amewaeleza wafanyabiashara wadogo na wakulima wa kahawa  jijini Dar es Salaam leo Machi 29, 2022 kuwa mikataba inasaidia uhakika wa biashara na kuongeza faida kwa kuwa inapunguza  changamoto zinazoweza kuibuka wakati wakiendesha biashara hiyo na kampuni za ununuzi za kimataifa. 

“Kila unapoingia mkataba na wanunuzi soma kwa makini kama utakufaidisha katika biashara yako. Biashara ya kahawa ni mikataba, hakikisha unaelewa inavyofanyika,” amesema Nsibirwa katika mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu.

Nsubirwa anayemiliki shamba la kahawa la Bussanyi amesema ili wafanyabiashara hao wafaidike kikamilifu, mnyororo wa thamani wa zao hilo ikiwemo mifumo ya usafirishaji na bei zipangiliwe vizuri kwa kuwahusisha wadau wote wa sekta ya zao hilo.


Soma zaidi:


Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa Market Access Programme (MARKUP) unaotekelezwa Tanzania unaolenga kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuboresha upatikanaji wa soko la mazao Umoja wa Ulaya (EU). 

Mshauri Mwandamizi wa Ufundi Kanda ya Afrika Mashariki wa MARKUP, Safari Fungo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati Tanzania kuwa na utaalamu wa biashara ya kuuza nje ya nchi na waweze kutumia soko la Umoja wa Ulaya. 

Fungo amesema mafunzo hayo yatawanufaisha wafanyabiashara 25 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania ambao watapata mafunzo ya darasani ya siku mbili na safari ya nje kwa siku ya mwisho. 

Kahawa ni moja ya mazao makuu ya biashara nchini Tanzania ambayo yamekuwa yakisafirishwa kwa wingi nje ya nchi na kuingiza nchi mapato ya kigeni.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020, tani 64,000 za kahawa ziliuzwa nje ya nchi mwaka juzi na kuliingizia Taifa Sh336.8 bilioni.   

Kiasi hicho kilishuka kutoka tani 76,200 zilizouzwa mwaka mwaka 2019 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa kahawa iliyouzwa nje na janga la Corona (Uviko-19).

Mafunzo hayo yanawashirikisha wataalam katika biashara ya kahawa nchini Tanzania na kimataifa.

Mradi wa Markup nchini Tanzania unafadhiliwa na EU kuzisaidia biashara ndogo ndogo na za kati (SMEs) zinazofanya kazi katika sekta za viwanda vya kilimo, ikiwa ni pamoja na kahawa, chai, parachichi, kilimo cha bustani na viungo ili kufikia uwezo wa kimataifa wa kuuza nje. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW