Dk Mpango atoa angalizo kutoweka kwa fukwe Tanzania

November 24, 2022 6:03 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango  akizungumza jana Novemba 23, 2022 katika Kongamano la Jukwaa la Maendeleo Endelevu (GGP) lililofanyika jijini Mwanza. Picha | Mariam John.

Asema shughuli za binadamu zinaharibu fukwe ambazo ni kivutio cha watalii.

  • Awataka watendaji, wawekezaji kuokoa fukwe katika mikoa yao.

Mwanza. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewaagiza watendaji katika mikoa iliyo karibu na bahari na maziwa ikiwemo Mwanza kulinda na kuendeleza fukwe ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kukuza sekta ya utalii. 

Dk Mpango amesema haridhishwi na hali ya utunzaji wa mazingira hasa fukwe katika baadhi ya mikoa ikiwepo Tanga, Mbeya na Mwanza, Dar Es Salaam, Mtwara, Lindi , Mwanza, Pwani na visiwa vya Zanzibar .

“Bado hatujaweza kutumia kikamilifu fukwe hizi kwa ajili ya maendeleo kama ilivyo katika nchi nyingine.  Asilimia kubwa za fukwe zetu hazijaendelezwa zinakabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira unaotokana na ongezeko la shughuli za binadamu kando kando ya fukwe ikiwemo uchimbaji wa mchanga, utupaji taka ovyo ikiwemo taka maji na taka ngumu, ujenzi holela, uvuvi haramu kilimo na ufugaji holela,” amesema Dk Mpango.

Kiongozi huyo aliyekuwa akizungumza jana Novemba 23, 2022 katika Kongamano la Jukwaa la Maendeleo Endelevu (GGP) amewaagiza watendaji wa mikoa hiyo kuandaa na kuanza utekelezaji wa mipango mikakati ya uendelezwaji wa fukwe na maeneo ya bustani za mapumziko.

Pia amewataka wafanyabiashara kuwekeza kwenye maeneo ya fukwe ili kukuza utalii na uchumi wa Taifa.

“Wataalamu, wadau mbalimbali na Watanzania wote kila mmoja kwa nafasi yake ana nafasi ya kufanya linalowezekana kunusuru fukwe. Ni vizuri tuwe na mijadala mipana ambayo itachangia kuleta mabadiliko chanya na kuisaidia Serikali kuimarisha mifumo yake ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kuweza kuboresha misingi ya usimamizi utunzaji na uwekezaji bora wa fukwe,” ameeleza Dk Mpango.


Zinazohusiana:


Amewataka washiriki wa jukwaa hilo kutumia fursa hiyo kubadilishana maarifa na ujuzi kuhusu matumizi ya rasilimali na kubadili mitazamo juu ya namna bora ya kuwekeza katika fukwe za bahari, maziwa na mito ili kuleta faida za kiuchumi na kukuza mchango wake katika pato la Taifa na maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, Serikali imesema katika hatua za kuendeleza mazao ya utalii nchini, itabainisha maeneo ya fukwe 136 katika maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa kwa ajili ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli za utalii. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23 alisema wamebaini maeneo yenye fursa za uwekezaji wa shughuli za utalii pembezoni mwa bahari ya Hindi katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. 

“Lengo ni kuyasajili maeneo hayo kama Kanda Maalum za Kiuchumi za Utalii kupitia Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje – EPZA,” alisema Dk Chana. 

Wizara ya Maliasili na Utalii ilifanya mkutano na wadau Jijini Dar es Salaam Februari, 2022 kwa lengo la kujadili uendelezaji wa maeneo hayo.

“Hatua hii itachochea ukuaji na uendelezaji wa shughuli za utalii wa fukwe, meli na michezo ya kwenye maji katika maeneo ya fukwe nchini,” alisisitiza waziri huyo. 

Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameeleza kuwa serikali itaendelea kutunza fukwe ili zitumike kama sehemu ya utalii.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW