Dk Mpango awataka wadau kutafuta suluhu ya changamoto za kimazingira

September 9, 2024 5:06 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema nchi inalia kutokana na uharibifu wa mazingira na kutaka kupatikana kwa suluhisho endelevu.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewataka wadau wote wa mazingira nchini kushirikiana kuibua na kupendekeza suluhisho endelevu kwa changamoto za kimazingira ili kupambana na uharibifu unaoendelea.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa kitaifa kuhusu mazingira uliofanyika Dodoma leo Septemba 9, 2024 ameelezea kwa kina hali mbaya ya mazingira nchini, akitarajia mkutano huo kuzaa suluhu ya kudumu.

“Ni matarajio yangu kuwa mkutano huu utasaidia kuainisha na kupendekeza njia zinazofaa kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mazingira pamoja na kutatua changamoto zilizopo…watoa mada mjikite kuwawezesha na kuhamasisha washiriki kuibua suluhu za changamoto za kimazingira zilizopo,” amesema Dk Mpango.

Kwa mujibu wa taarifa ya mazingira 2024 hali ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira hairidhishi ikisababishwa kwa kiasi kikubwa na tabia za watu hususan ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu ambapo wastani wa hekta 24,151 hupotea kwa mwaka.

Miongoni mwa tabia hatarishi za binadamu kwa mazingira alizozianisha  Dk Mpango ni kuendelea kwa utumiaji wa nishati chafu ya kuni na mkaa, uvunaji wa rasilimali misitu usioendelevu, kilimo na ufugaji holela usiozingatia uwiano kati ya mifugo na maeneo ya malisho.

Ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa matumizi ya mkaa na kuni katika kaya zote Tanzania Bara yamefikia asilimia 67.

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu au kaya sita kati ya 10 zinatumia nishati hiyo kwa ajili ya mapishi huku asilimia 25 wakitumia majiko ya mkaa na asilimia 8.1 majiko mengine.

Hali ni mbaya zaidi kwa kaya zilizopo vijijini ambapo asilimia 88 zinatumia kuni kama chanzo kikuu cha mapishi, kulinganisha na asilimia 6 ya kaya zinazotumia nishati hiyo mjini.

Kutokana na hali hiyo Dk Mpango amesema bado kazi kubwa inatakiwa kufanywa na wadau wa mazingira ili kuokoa mwenendo mbaya uliopo wa hali ya mazingira kwani kwa mfululizo ripoti nne zilizotolewa na ofisi yake zinaonesha bado kuna uharibifu mkubwa unaendelea licha ya kampeni na jitihada za utunzaji.

Changamoto zinazokwamisha utunzaji wa mazingira zatajwa

Kwa mujibu wa Dk Mpango miongoni mwa changamoto zinazokwamisha utunzaji wa mazingira ni pamoja na sheria kinzani ikiwemo ile iliyounda Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambayo bado inafanya mkaa kuwa chanzo cha mapato.

Nyingine ni kasi ndogo ya kupanda miti ikilinganishwa na kasi ya ukataji, mbinu hafifu za kutoa elimu kwa umma, idadi ndogo ya vitalu vya miche ya miti visivyotosheleza mahitaji na kutokutunzwa kwa miti iliyokwisha kupandwa.

“Lakini pia ziko tuhuma kuwa wafanya biashara wa mkaa baadhi yao ni wafanya maamuzi na wana maslahi binafsi, vilevile mahitaji ya kilimo na ufugaji yanashindana na mahitaji ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi, teknolojia za kijani hazipatikani kwa urahisi na zinapopatikana ni ghali mno…

…wenye kipato kidogo wanashindwa kumudu teknolojia za kijani na Serikali kama (ya) nchi yetu ina uwezo mdogo wa kutoa ruzuku, kwa hiyo hizi zote ni changamoto ambazo mkutano huu utazijadili na kuja na mapendekezo ya namna ya kwenda mbele ili Tanzania ishamiri iache kulia kutokana na uharibifu wa mazingira,” ameeleza Dk Mpango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks