Dk Mpango ataka hatua kali zichukuliwe wanaohujumu ujenzi reli ya kisasa
- Askari wa Jeshi la Polisi nao watajwa kushiriki kwenye wizi wa vifaa vya ujenzi.
- Makamu wa Rais Dk Mpango aagiza washughulikiwe kwa sheria za kijeshi.
- Mafuta, saruji na nondo vyatajwa kuibwa zaidi.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini kufuatilia na kuwakamata watu wote wanaohusika na wizi wa vifaa katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaoendelea mkoani Shinyanga.
Makamu wa Rais aliyekuwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa SGR kipande cha Tabora-Isaka leo Januari 18, 2023 amewaambia Watanzania kuwa anazo taarifa za wizi wa vifaa kama mafuta, nondo, na saruji jambo linalokwamisha juhudi za Serikali.
“Hawa wezi ni wahujumu wa uchumi, hawatutakii mema kama taifa, naviagiza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viwasake wahusika wote, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria, ” amesema Dk Mpango.
Mpango ameongeza kuwa wamebaini uwepo wa mtandao wa uhalifu ambao wananunua mali hizo na kwenda kuziuza sehemu nyingine kama migodini ambao nao wanatakiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Soma zaidi
Maaskari nao wapo
Licha ya uhalifu huo kutajwa kufanywa na waajiriwa wa mkandarasi wakiwemo madereva, waongoza mitambo na wakazi wa maeneo jirani, Makamu wa Rais amesema wapo baadhi ya askari ambao wamekuwa wakishiriki wizi huo.
“Wapo baadhi ya askari wachache ambao wanashiriki kwenye uhalifu huu, sio tu naagiza wakome bali nao wasakwe na wakamatwe na washughulikiwe kwa mujibu wa sheria ikiwemo sheria za kijeshi,” amesema Mpango.
Itakumbukwa Januari 13 mwaka huu Makamanda wa Polisi Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mwanza walitoa onyo kali kwa watu wanaohujumu ujenzi wa mradi wa SGR kipande cha Isaka hadi Mwanza ambapo baadhi ya vitu kama mafuta na pikipiki zilikamatwa katika oparesheni mbalimbali zinazoendelea kufanywa.
Kipande cha reli cha Tabora -Isaka kinachojengwa na kampuni ya Uturuki ya Yepi Merkezi kina urefu wa kilomita 165 ambazo zitagharimu Dola za Marekani milioni 900.1 sawa na Sh2.09 trilioni.
Ujenzi wa kipande hicho unafanya jumla ya fedha ambazo zitatumika kwenye ujenzi wa SGR kufikia Sh23.3 trilioni ambapo mpaka sasa Serikali imeshalipa jumla ya Sh7.7 trilioni.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amewaambia Watanzania kuwa kukamilika kwa miradi ya ujenzi wa SGR kutachochea kasi ya ukuaji uchumi kwani usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi utakuwa wa haraka zaidi kuliko sasa.
“Miradi hii ikikamilika, kusafirisha mzigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakuwa ni kati ya masaa 26 hadi 36 tofauti na sasa ambapo huchukua wastani wa siku 30, “ amesema Mbarawa.
Tangazo:

Latest