Tanzania kuimarisha vituo vya unenepeshaji mifugo
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akikagua maendeleo ya Kituo Atamizi cha Mabuki kinachotumika kunenepesha ng’ombe wa nyama pamoja na mpango wa mafunzo ya ujasiriamali kupitia sekta ya mifugo kilichopo Misungwi mkoani Mwanza Aprili 11, 2023. Picha | Ofisi ya Makamu wa Rais.
- Kwa sasa Tanzania ina vituo nane.
- Vitasaidia kuongeza thamani ya mifugo zikiwemo ng’ombe.
- Vitaongeza kipato na ajira kwa Watanzania.
Mwanza. Serikali imesema itaongeza nguvu na fedha kwenye vituo atamizi vya kunenepesha mifugo zikiwemo ng’ombe ili viweze kuleta tija kwa vijana na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akizungumza baada ya kutembelea mradi wa vijana wa kunenepesha ng’ombe katika kituo cha Mabuki Aprili 11, 2023 amesema Serikali inataka kuona mabadiliko kwenye sekta ya mifugo ambapo kupitia vituo hivyo wafugaji watapata elimu ya namna ya ufugaji bora.
” Tunataka kuona wafugaji wanaacha kufuga kizamani na sasa waanze kufuga kisasa ambapo mfugaji mwenye ng’ombe mmoja aone thamani yake tofauti na ilivyo sasa ambapo wanafuga kiholela na isiyo na tija,” amesema makamu wa Rais.
Amesema ni aibu kwa Taifa ambalo ni la tatu barani Afrika kwa ufugaji lakini mifugo yake haina tija.
“Kuanzishwa kwa vituo hivi atamizi ni ukombozi kwa Taifa, ni hatua ya kupongezwa na kusifiwa ambapo sio tu kwamba Taifa litafanikiwa kuuza nyama bora na mifugo nje ya nchi lakini pia vijana wanaohitimu elimu watajipatia ajira,” amesema Dk Mpango.
Amesema inastajabisha kuona maprofesa wanafundisha kilimo na ufagaji lakini wao hawaishi kwenye huo ufugaji hivyo kuanzishwa kwa vituo hivi inatoa picha kile kinachofundishwa vyuoni kinakuja kufanyiwa kazi kwenye jamii.
Makamu wa Rais amepongeza Wizara ya mifugo kwa kuja na wazo hilo na kwamba changamoto za kituo cha Mabuki zilizowasilishwa ikiwemo ukosefu wa umeme, mashine za kuchanganyia chakula na roli la kubebea mifugo kwenda mnadani zitafanyiwa kazi ili kuwasaidia vijana hao kufanya kazi kwenye mazingira mazuri.
“Nimeona kwa macho kazi nzuri inayofanyika hapa kwa kweli nawapongeza sana hata hiyo bajeti mliyoomba hapa naweza nikaenda kwa Rais hata kwa kumpigia magoti ili aweze kutatua changamoto hizo,” amesema Dk Mpango.
Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema jumla ya vituo atamizi vinane vimeanzishwa nchini ili kuwasaidia vijana kujipatia ajira na kuongeza kipato chao.
Pia ng’ombe 2,150 zimenunuliwa na vijana 240 wamejiajiri kwenye vituo hivyo.
Katika kituo cha Mabuki tayari vijana 85 wamepatiwa mafunzo ya namna ya unenepeshaji wa mifugo ili waweze kuongeza thamani ya mifugo na kujipatia kipato.
Latest