Masomo ya sayansi yakimbiza matokeo ya kidato cha sita 2023

July 14, 2023 4:47 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaongoza kwa ufaulu kwa asilimia 74.9
  • Tahasusi za KLC, KLI na KLA zashika mkia.

Dar es Salaam.Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2023 huku masomo ya sayansi yakiongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi waliofaulu kushinda masomo mengine.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Ally Mohamed amesema aliyekuwa akitangaza matokeo ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2023 leo Julai 13, 2023 amesema masomo ya sayansi yameongoza kwa ufaulu kwa asilimia 74.9.

“Kwa kuzingatia idadi ya watahiniwa zinazoonyesha kuwa idadi kubwa ya waliopata daraja la kwanza na la pili ipo katika tahasusi ya sayansi ikifuatiwa na tahasusi za sanaa,” amesema Dk Mohamed.

Kwa mujibu wa matokeo hayo wanafunzi 28,236 waliofanya mitihani ya tahasusi za PCM (Fizikia, Kemia na Hesabu), PCB (Fizikia, Kemia na Biolojia) na PGM (Fizikia, Jografia na Hesabu) wamefaulu kwa daraja la kwanza na la pili.

Kati ya hizo tahasusi ya PCM ina ufaulu mzuri zaidi ambapo asilimia 45 ya wanafunzi waliofanya mitihani ya masomo hayo wamepata daraja la kwanza. Ikifuatiwa na  tahasusi ya PCB na PGM zilizopata ufaulu wa asilimia 35 na 34 mtawalia.


Zinazohusiana


Masomo ya sanaa nayo moto

Mbali na masomo ya sayansi, DK Mohamed amesema masomo ya sanaa nayo yamefanya vizuri ambapo jumla ya wanafunzi 24, 890 wamefaulu mitihani hiyo. Katika masomo hayo tahasusi za lugha ikiwemo HKL imefanya vizuri zaidi kulinganisha na tahasusi nyingine za sanaa.

“Tahasusi hii ya HKL (Historia, Kiswahili na Lugha) ndiyo tahasusi yenye ufaulu mkubwa zaidi ambapo watahiniwa 6,747 sawa na asilimia  41.4 wamepata daraja la kwanza,” amesema  Dk Mohamed.

Hiyo ni sawa na kusema karibu nusu ya watahiniwa 16,296 waliofanya mtihani katika  tahasusi hiyo mwezi Mei mwaka huu wamepata daraja la kwanza, ambapo kwa mujibu wa Dk Mohamed idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko tahasusi nyingine zilizofanya mtihani hiyo.

Tahasusi nyingine za sanaa zilizofanya vizuri katika matokeo hayo ni GKL (Jografia, Kiswahili na Lugha)  yenye ufaulu wa asilimia 18. 7 na KLF (kiswahili,  lugha na kifaransa) yenye asilimia 39.2 waliopata daraja la kwanza.

Aidha tahasusi za KLA(Kiswahili, Lugha na Kiarabu), KLI (kiswahili,lugha na Elimu ya kiislamu) pamoja na KLC (Kiswahiili,Lugha na Kichina) zimefanya vibaya katika matokeo hayo.

Mathalani tahasusi ya KLA yenye wanafunzi 18 tu waliopata daraja la kwanza kati ya wanafunzi 87 waliofanya mtihani huo.

Wanafunzi 11 kati ya 39 waliofanya mtihani wa KLI wamepata daraja la kwanza na wanafunzi 9 kati ya 19 kutoka tahasusi ya KLC ndio waliopata daraja la kwanza.

Enable Notifications OK No thanks