Maumivu: Necta yafuta matokeo ya watahiniwa 11 kidato cha sita 2023

July 13, 2023 11:04 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kufanya udanganyifu kidato cha sita.
  • Waliofutiwa matokeo wapungua kutoka 15 wa mwaka jana.
  • 169 wazuiliwa matokeo yao, kufanya upya mtihani 2024.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 11 wa kidato cha sita baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu katika mtihani uliofanyika Mei mwaka huu wa 2023. 

Idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka huu imepungua ikilinganishwa na 15 waliofutiwa mwaka jana na 27 waliofutiwa mwaka 2021, jambo linalodhihirisha kuwa vitendo hivyo vilivyo kinyume na Sheria vinadhibitiwa. 

“Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 11.  Nane wa shule na watatu wa kujitegemea wa mtihani wa kidato cha sita ambao walibainika kufanya udanganyifu,” amesema  Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Ally Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2023 leo Julai 13, 2023.


Zinazohusiana

Ufaulu matokeo kidato cha sita 2023 waongezeka kiduchu

Matokeo kidato cha sita 2023 haya hapa


Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) cha Sheria ya Necta sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu ch 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani mwaka 2016 ambazo zinakataza vitendo vyovyote vya udanganyifu wakati wa mitihani.

Matokeo yaliyozuiliwa  

Necta pia imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 169 wakiwemo 153 wa mtihani kidato cha sita, nane walimu daraja A na nane wa stashahada ya walimu wa sekondari ambao walipata matatizo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya masomo yote au kwa idadi kubwa ya masomo.

“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mitihani kwa masomo ambayo hakufanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 30(1) cha Kanuni za Mitihani,” amesema Dk Mohamed.

Enable Notifications OK No thanks