Jinsi ya kuongeza ushiriki wa vijana kwenye uchaguzi Tanzania

September 18, 2024 2:02 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na utoaji wa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo nyimbo na maigizo.

Arusha. Wakati Tanzania ikijiandaa na Uchaguzi wa  Serikali za Mitaa mwishoni mwa  2024 na ule wa Serikali kuu unaotarajia kufanyika mwakani baadhi ya wadau wa sekta binafsi wameanisha mbinu zitakazosaidia kuongeza ushiriki wa vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura ikiwemo kutoa elimu.

Vijana ni miongoni mwa makundi muhimu yanayotegemewa kuchochea kasi ya maendeleo kutokana na ushiriki wake kwenye nyanja mbalimbali za kijamii kama uchumi, na biashara na siasa.

Licha ya Tanzania kuwa na zaidi ya asilimia 30 ya vijana, kundi hilo bado limelalamikiwa kuwa na ushiriki mdogo katika masuala ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania ina asilimia 34.5 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 huku miongoni mwao kwa mujibu wa sheria ya Tanzania wakiruhusiwa kupiga kura na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Baadhi ya wadau wa maendeleo wametumia midahalo katika madhimisho ya wiki ya Azaki yaliyofanyika jijini Arusha kutoa mapendekezo yanayoweza kuchochea ushiriki wa vijana katika masuala ya uchaguzi ikiwemo kutoa elimu juu ya umuhimu wa ushiriki wao katika jambo hilo.

Abella Bateyunga, Mkurugenzi Mtendaji kutoka taasisi ya Tanzania Bora Initiative amesema miongoni mwa mbinu inayoweza kutumika ni kutoa elimu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo maigizo na nyimbo.

‘Kupitia program zetu (nyimbo na maigizo) tumeweza kufikia vijana wengi katika uchaguzi wa mwaka 2020 tukitoa elimu ya umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na kweli mbinu hiyo ilitusaidia,” amesema Bateyunga Septemba 13, 2024 alipokuwa akichangia katika mdahalo huo.

Mchangiaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Joel Nkya amesema mbinu nyingine inayoweza kuchochea ushiriki wa vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ubunge ni kubadilisha sera ya viti maalum bungeni na kutoa nafasi kwa vijana wanaoichipukia kuchukua nafasi hizo.

“Tukiwa na ukomo wa special seat (viti maalum) inaweza kusaidia lakini pia kwanini tusiwe na viti maalum vya vijana ambapo lengo kuu ni kuwajengea uwezo lakini tunaongeza idadi kubwa ya vijana bungeni nanafasi nyingine mbalimbali,” amesema Nkya.

Baadhi ya washiriki wa mdahalo wa vijana na uchaguzi katika wiki ya azaki iliyofanyika jijini Arusha.Picha|TBI/instagram.

Hata hivyo, tayari kuna nafasi moja ya mbunge wa viti maalum wa vijana inayoshikiliwa na Ng’wasi Kamani (CCM) ambayo wadau hao wa sekta binafsi wamekiri kuwa haitoshi kuwakilisha vijana wote waliopo nchini.

Kwa upande wake Janeth Mbene, Mkurugenzi wa Tanzania Women Empowement (TAWEN) ambaye pia aliwahi kuwa mbunge (CCM) kati ya mwaka 2015 hadi 2020 amesema kitakachoongeza ushiriki wa vijana katika uongozi ni fedha zitakazowawezesha kufanya kampeni katika maeneo mengi zaidi na kushawishi wananchi kuwachagua, fedha hizo zinazoweza kutoka kwa vijana wenyewe au mashirika na taasisi. 

“Chagueni vijana ambao wapo tayari wachangieni kama suala ni funding (fedha) hiyo ndiyo njia pekee itkayowasaidia…wote sisi tulichangiwa ndio tukaingia,” amesema Janeth.

Aidha, Francisca Mboya ambaye ni miongoni mwa wachangiaji katika mdahalo huo ameshauri kuundwa kwa kanzi data ya vijana wanaotia nia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kuwaunga mkono na kuwabebesha ajenda zinazohusu kundi hilo wanazotakiwa kuzifanyia kazi wakichaguliwa.

Licha ya maoni hayo, hivi karibuni Serikali ilizindua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 maboresho ya mwaka 2024 ikiwa na lengo la kutatua baadhi ya changamioto zilizoibuliwa na wadau hao wa sekta binafsi ikiwemo kuundwa kwa baraza la vijana.

“Vijana wamekosa maeneo ya kueleza changamoto zao, vijana walikosa watu wa kuwasikiliza, vijana walikosa mfumo wa kuwasilisha changamoto zao na kuzitafutia majawabu kwa pamoja…

…Ujio wa sera hii ya vijana na uundwaji wa baraza hili la vijana ni dhahiri kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha changamoto zote zinatafutiwa majawabu,” alisema Ridhiwani Kikwete Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Vijana Kimataifa Agosti 12, 2024.

Aidha, sera hiyo mpya pia itawatambua vijana katika nyanja zote za uzalishaji mali ikiwemo wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

Enable Notifications OK No thanks