ZEC yasitisha uchaguzi jimbo la fuoni kutokana na kifo cha Abbas Mwinyi
- Atazikwa leo Septemba 26, 2025 nyumbani kwao Mangapwani mkoa wa Kaskazini Unguja.
Arusha. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC ) imetangaza kusitishwa kwa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi B, kufuatia kifo cha Kapteni Abass Ali Mwinyi, mgombea wa CCM.
Taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Fuoni Miraji Mwadini Haji iliyotolewa Septemba 25, 2025 inabainisha kuwa uchaguzi katika jimbo hilo utasitishwa hadi pale itakapotangazwa tarehe nyingine.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume kwa notisi itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali itapanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea na taratibu za uchaguzi wa Ubunge katika jimbo husika zitaanza upya,” imesem taarifa ya Haji.
Aidha, INEC imesema itahifadhi nafasi za wagombea walioteuliwa kihalali iisipokuwa iwapo mgombea atajitoa huku kampeni za ubunge zikitarajiwa zitarejea baada ya uteuzi wa mgombea mpya.
Kapteni Abbas Mwinyi ambaye pia ni kaka wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibari Hussein Mwinyi alifariki dunia Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba, Unguja.
Enzi za uhai wake Abbas alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa Chama cha Mapainduzi (CCM) akiwa mbunge wa Fuoni kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020.
Kaba ya kufikwa na umauti Abbas alikuwa akitetea nafasi yake ya ubunge katika Jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi B.
Abbas ambaye pia ni rubani atazikwa leo Septemba26, 2025 nyumbani kwao Mangapwani mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya swala ya mchana.
Viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Tanzania akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wamefika kumpa pole Rais Mwinyi nyumbani kwa marehemu Bweleo, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Latest