Zao la alizeti: Utalii, kilimo vinapokutana pamoja

November 10, 2021 11:36 am · Nasibu
Share
Tweet
Copy Link
  • Hutumika kutengeneza mafuta ya kupikia.
  • Maua yake ni kuvutio kwa watalii.
  • Ni fursa ya kukuza kipato kwa vijana na wanawake.

Wanasema bustani haikamiliki bila maua na huo ni ukweli usiopingika, maua huongeza mvuto na maua mengine yana tija kwenye lishe yetu pia. 

Napenda nikujuze kuwa zaidi ya asilimia 99 ya matunda yote duniani hutokana na maua.

Moja ya vigezo vyangu vya kutafuta mke wa kuoa ni kuwa mwanamke lazima apende na ajue jinsi ya kuhudumia bustani ya maua, tena akiweka na maua ya alizeti atanifurahisha sana.

Alizeti ni ua? Lina upekee gani katika sekta za kilimo na utalii? Twende pamoja.

Asili ya ua la alizeti ni Amerika ya Kaskazini na lilikuwa likiota kama ua pori huku likitoa bidhaa kama dawa na mafuta hadi kuanza kulimwa kibiashara miaka ya 1500 iliyopita na wazungu waliolowea Marekani na mwishowe ua hilo kusambaa duniani kote.

Ua hili lenye kufanana na sahani, lina rangi ya njano kwenye petali na kahawia iliyokolea katikati kwenye mbegu. Ua hili kwa Kiingereza linaitwa ‘Sun Flower’ na ni kutokana na sura yake kufanania muonekano wa jua.

Lakini pia kwa kifaransa linaitwa ‘Tournesol’ ikimaanisha ‘kugeukia jua’ ambayo ni sifa nyingine ya ua hili. Ua hili lina uwezo wa kugeukia upande ambao mionzi ya jua hutokea.

Alizeti ni miongoni mwa mazao ya mbegu za mafuta. Picha| meriç tuna on Unsplash

Sifa zake

Mmea wa alizeti unaweza kuwa na urefu wa hadi futi 12, sawa urefu wa watu wawili kwenda juu. Alizeti refu kuliko duniani lilikuwa na urefu wa futi 30, lilioteshwa nchini Ujerumani.

Katikati ya ua la alizeti kuna mbegu zisizopungua elfu moja, mbegu hizo ambazo zikikamuliwa hutoa mafuta ya kupikia ya alizeti yenye vitamin A na D na yasiyo na lehemu, yani Kolestro.

Kazi ya alizeti katika shughuli mbalimbali

Alizeti ambalo limeshavunwa mbegu linaweza kutumika kama dodoki la kujisugulia mwili wakati wa kuoga.

Alizeti pia hufanya kazi nzuri ya kunyonya miyonzi ya sumu iliyomo kwenye hewa na kwenye udongo. Kwa mfano, nchini Japan zaidi ya mimea ya alizeti ilipandwa ili kupambana na mionzi ya nyuklia baada ya Tsunami kubomoa matenki ya Uranium kwenye kitongoji cha Fukushima mwaka 2011.

Alizeti linavutia sana nyuki hivyo kama mfugaji wa nyuki akipanda maua haya yanaweza kumuongezea faida katika mavuno yake ya asali.

Barani Afrika, zao la alizeti lililetwa na wakoloni na Tanzania ni moja ya nchi 10 duniani zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao hili. Zaidi ya tani 350,000 huvunwa kila mwaka. 

Maua ya alizeti ni kivutio cha watalii hasa wanaopenda kupiga picha zenye maua yanayovutia. Picha|  Antonino Visalli on Unsplash

Alizeti ni zao la utalii duniani

Katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, Singida na Kilimanjaro ni baadhi ya sehemu ambazo maua haya hupatikana kwa wingi, lakini je, alizeti na muonekano wake wa kuvutia linaishia tu kuwa zao la kibiashara afu basi?

Nchi kama Marekani na Ukreini ni moja kati ya nchi za kwanza zilizoona fursa ya utalii ndani ya ua la alizeti. 

Kwa kuwa maua haya yanavutia machoni na wanawake wakipiga nayo picha hupendeza sana, basi mataifa hayo yamebuni aina ya utalii uitwao utalii wa kilimo ambao unahusisha watalii kutembelea mashamba ya alizeti, kujionea jinsi kilimo hicho kinavyofanywa na pia kupiga picha ambazo zitabakia kuwa kumbukumbu za kudumu milele.

Utalii wa alizeti pia huangukia kwenye utalii wa maua kama ambao yaliyopo kwenye hifadhi ya Taifa ya Kitulo japokuwa maua ya Kitulo ni uoto wa asili.

Je, wewe ni mkulima wa alizeti na ungependa kupata watalii watakaolipia ziara za shambani kwako? Fursa iko wazi hiyo! Tutafutane! Nchi yetu hii ni dili!

Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya www.nasibumahinya.com.

Enable Notifications OK No thanks