Namna ya kuishi na mtoto mwenye Sikoseli
- Ni pamoja na kuhakikisha anapata huduma zote za msingi ikiwemo lishe kama watoto wengine.
- Pia mzazi ni muhimu kumuepusha na michezo mizito au shughuli zinazomchosha mwili kupita kiasi.
Licha ya kuwa idadi ya watu wanaobainika kuzaliwa na sikoseli ama selimundu kuongezeka nchini, baadhi ya wazazi hawafahamu namna ya kuwalea watoto wao wenye maradhi hayo yanayojumuisha maumivu makali mwilini.
Katika sehemu ya kwanza na ya pili ya series (mfululizo) wa makala haya tuliangaza visababishi vya sikoseli ama kwa jina jingine selimundu, dalili na namna mashujaa wa sikoseli wanavyoishi.
Katika makala hii ya mwisho tutaangazia njia zitakazowasaidia wazazi kuwalea watoto wanaougua selimundu ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora kwa kuwa kumlea mtoto mwenye ujonjwa huo ni gharama hivyo kuleta maumivu zaidi kwa familia za kipato cha chini.
Dk Deogratius Soka, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Tanzania Sickle Cell Disease Alliance aliiambia Nukta Habari kuwa wazazi wa watoto wenye sikoseli wanapaswa kuwa waangalifu sana katika maisha ya kila siku ya mtoto.
Mnyweshe mtoto maji mengi
Jambo la kwanza ni kuhakikisha mtoto anakunywa maji ya kutosha kila siku ili kuzuia upungufu wa maji mwilini ambao unaweza kuchochea maumivu makali.
Upungufu wa maji mwilini ni miongoni mwa vichochezi vya maumivu kwa mgonjwa wa sikoseli.

Ni muhimu pia kuhakikisha mtoto anakunywa vinywaji vingine salama kama maziwa au juisi ya matunda. Juisi hiyo inaweza kuwa juisi ya tikitimaji, machungwa, nanasi au miwa ili kuepuka upungufu wa maji mwilini, jambo ambalo linaweza kuongeza maumivu na matatizo mengine yanayohusiana na sikoseli.
Mkinge na baridi kali
Baridi kali huchochea unyongefu wa mtoto na kufanya mishipa yake ikakamae jambo linalochochea na kuamsha maumivu mwilini.
Dk Soka anasema ni muhimu kumlinda mtoto dhidi ya baridi kali kwa kumpa mavazi ya joto hasa wakati wa usiku au msimu wa baridi.
Vilevile, joto la kupindukia na vumbi la baridi linaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini na msongo wa mawazo, hivyo ni vyema kuhakikisha mazingira ya mtoto ni tulivu, si baridi kali wala joto kali.
Mtoto asichoke sana
Mara nyingi watoto hupenda kucheza sana kiasi cha kuchoka miili yao. Sikoseli na uchovu havipatani.
Wataalamu wa afya wanashauri kuwa mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto wake hachoki kupita kiasi hivyo, anapaswa kuepuka michezo mizito au shughuli zinazomchosha mwili kupita kiasi.
Kufanikisha hilo, mtoto mwenye sikoseli anapaswa kufuatiliwa ratiba yake ya kucheza au kufanya kazi kuhakikisha hazidishi kiwango kinachotakiwa.
Fuatilia maendeleo ya mtoto hospitalini
Baadhi ya wazazi hawapendi kwenda hospitalini mpaka mtoto aumwe. Hapana. Hii si sawa katika malezi ya mtoto mwenye sikoseli.
Wazazi, Dk Soka anasema, wanapaswa kuwa na ratiba ya kufuatilia afya ya mtoto mara kwa mara hospitalini na kuhakikisha anapata lishe bora pamoja na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Mpe mtoto lishe bora
Hatua nyingine ni kuhakikisha mtoto wa anapata lishe sahihi kama wanavyopata watoto wengine ikiwemo kuzingatia muongozo sahihi wa ulaji wa makundi yote ya chakula.
Lishe hiyo inapaswa kuwa na mchanganyiko wa vyakula vyenye nyuzi, protini, na virutubisho muhimu kama zinki na folate (vitamini B), ambavyo husaidia kuimarisha seli nyekundu za damu, kurejesha damu inayopotea kutokana na ugonjwa, na kupunguza hatari ya anemia.
Mifano ya vyakula vyenye zinki ni pamoja na karanga, nyama ya kuku au ng’ombe, samaki, maharage, na nafaka kamili kama mchele wa kahawia au quinoa.

Vyakula vyenye folate ni pamoja na mboga za majani kama spinachi na broccoli, viazi vitamu, karoti, na matunda kama papai na strawberries.
Aidha, vyakula vilivyoimarishwa na folate kama chakula cha mahindi, mkate, mchele, na unga pia vinaweza kusaidia.
Kwa kumpa mtoto lishe kamili, yenye virutubisho vyote muhimu husaidia mwili wake kushughulikia changamoto za sikoseli, kuimarisha kinga yake na kuboresha afya yake kwa ujumla.
Muanzishie mtoto matibabu ya kinga mapema
Tovuti ya Hopsitali ya Watoto ya Benioff ya nchini California (Benioff Children Hospital) inabainisha kuwa mara tu mtoto anapogundulika kuwa na sikoseli, ni muhimu kuanza matibabu ya kinga hata kama bado hana dalili.
Tovuti hiyo inaeleza kuwa kuanzia umri wa miaka miwili hadi mitatu na kuendelea hadi miaka 16, mtoto anatakiwa kufanyiwa kipimo cha kila mwaka cha Transcranial Doppler ili kupima hatari ya kupata kiharusi na kumfanyia kipimo cha MRI mara tu anapofikisha umri wa miaka mitano.
MRI ni kipimo kinachotumia mashine yenye sumaku yenye nguvu ya kuzalisha picha za ndani ya mwili wako.
Zungumza na mtoto juu ya ugonjwa wake
Mbali na kumhudumia, ni vema ukamweleza ukweli kuhusu hali yake. Tovuti ya St Jude Children Research Hospital inasema kumsaidia mtoto kuelewa ugonjwa wake kutamrahisishia kuilewa vizuri hali ya afya yake jambo litakao mfanya aweze kujirinda vema.
Katika kutekeleza hili mzazi anapaswa kuwa na mawasiliano ya wazi na mtoto, kujibu maswali yake kwa lugha inayofaa na kumfahamu hisia zake ikiwa na pamoja na kutumia mifano rahisi au vitabu vinavyoelezea hali kama yake.

Kuanzia umri wa miaka mitatu, watoto huwa wanaanza kuzungumza kwa sentensi fupi hivyo kwa kiasi kikubwa huelewa mambo mengi na kwa wakati huu zungumza na mtoto wako kuhusu ugonjwa wa sikoseli na mpe nafasi ya kukuuliza maswali.
Jambo la muhimu kujua ni kwamba hakuna shida kama hujui majibu yote ila kuzungumza naye kunampa nafasi ya kuzungumzia hofu zake na hisia zake.
Kwa mtoto kutambua kuwa ugonjwa alionao ni ugonjwa anaoweza kuugua mtu yoyote humsaidia kumjengea kujiamini na kujihisi wa kawaida kama watoto wengine.
Mkinge mtoto na maambukizi ya magonjwa
Ni muhimu kwa mzazi/mlezi kumsaidia mtoto kuzuia maambukizi kwa njia rahisi kwa kumuepusha na watu wenye changamoto za kiafya hasa wale wenye mafua, kikohozi au homa.
Pia, mfundishe kunawa mikono mara kwa mara, hasa kabla ya kula, baada ya kutoka chooni, au baada ya kucheza.
Aidha, hakikisha mtoto anapata chanjo zote muhimu, ikiwemo chanjo ya ‘pneumococcal’ inayomkinga dhidi ya nimonia na magonjwa mengine huku ukiweka utaratibu wa kumfanyia vipimo vya kawaida kama kipimo cha homa ya ini, ili madaktari waweze kugundua mapema iwapo kuna tatizo lolote.
Una maoni au unataka kutushirikisha jambo lolote kuhusu ugonjwa sikoseli usisite kucomment au kututumia ujumbe wa simu au WhatsApp kupitia 0677 088 088.
Latest



